Business

header ads

UNDANI KANUNI MPYA ZA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
Baada ya kuunganisha mifuko minne ya hifadhi ya jamii, Serikali imetoa kanuni mpya zinazozuia fao la kukosa ajira.

Kwa mwanachama atakayeachishwa kazi, kanuni zinasema atalipwa fao la kutokuwa na ajira ambalo ni sawa na theluthi moja (asilimia 33.3) ya mshahara aliokuwa anapokea akiwa kazini.

Malipo hayo, kanuni zinasema: “Yatadumu hadi miezi sita ndani ya mwaka mmoja mpaka mwanachama huyo atakapopata ajira nyingine. Endapo hatapata ajira mpya, mwanachama hatalipwa kwa zaidi ya miezi 18 kwa muda wote wa utekelezaji wa taaluma yake.”

Baada ya Bunge kupitisha Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na kuiunganisha mifuko ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF na kuunda mmoja kwa ajili ya watumishi wa umma ambao umeanza kufanyakazi kuanzia Agosti Mosi, kanuni mpya zimepitishwa.

Kabla ya kuunganishwa kwa mifuko hiyo, kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu fao la kujitoa ambao hata hivyo, Serikali ilishikilia msimamo wake kwamba utaratibu huo haupo.
Agosti 17, Waziri Jenista Mhagama mwenye dhamana ya kazi na ajira nchini alisaini kanuni za Sheria ya Hifadhi ya Jamii kuruhusu kuanza kutumika kwake.

Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Kisaka alithibitisha akisema, “ni zenyewe. Zimepitishwa na zitaanza kutumika.”

Ikitokea mwanachama huyo hajapata ajira nyingine miezi 18 baada ya kupokea malipo ya kutokuwa na ajira, basi atatakiwa kubadili michango yake kwenda mpango wowote wa kuchangia kwa hiari aupendao.

Kiwango kitakachohamishwa kwenda mpango huo kitakuwa jumla ya michango yote kutoa pensheni aliyolipwa kipindi cha kukosa ajira. Mwanachama huyo ataendelea kuchangia mpango aliouchagua kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazousimamia.

Utaratibu wa fao la kukosa ajira linawahusu wale wanaofanyakazi za muda mfupi au za mkataba pia. Kwa mwanachama ambaye michango yake ni chini ya miezi 18 ambayo ni sawa na mwaka mwaka mmoja na miezi sita, kanuni zinasema anastahili malipo ya pamoja kiasi cha asilimia 50 baada ya kuachishwa kazi.

Endapo ataendelea kukosa ajira kwa miezi 18 baada ya kupokea asilimia 50 ya michango yake atatakiwa kujiunga na mpango wowote wa kuchangia kwa hiari atakaoupenda. “Kiasi kitachopelekwa kwenye mchango wa hiari kitakuwa kilichobaki baada ya malipo ya awali, asilimia 50,” zinabainisha kanuni hizo.

Kama ilivyokuwa awali, kanuni zinasema mwanachama atastahili pensheni endapo atakuwa amechangia kwa kipindi kisichopungua miezi 180 au miaka 15.

Zinasema yule atakayekuwa amechangia kwa kipindi hicho au zaidi lakini akaachishwa kazi kwa manufaa ya umma kabla ya kufikisha umri wa kustaafu, atalipwa kiinua mgongo lakini ataanza kupokea pensheni ya kila mwezi atakapofikisha umri unaokubalika.

Kanuni hizo zinatambua miaka 55 kuwa ndio umri wa kustaafu kwa hiari na 60 kwa mujibu wa sheria.

Na mwanachama atakayeachishwa kazi kabla ya kufikisha umri wa kustaafu lakini amechangia chini ya miaka 15 au miezi 180, atalipwa kiinua mgongo pekee.

Mwanachana ambaye amechangia kwa zaidi ya miezi 180 lakini hajafikisha umri wa kustaafu ila ameteuliwa kushika wadhifa wa kisiasa ambako kuna utaratibu maalumu kwa ajili yao, atalipwa kiinua mgongo wakati akisubiri kupokea pensheni atakapofikisha miaka 55.

Licha ya watakaoteuliwa ikitokea mwanachama amepunguzwa kazi, ofisi aliyokuwa anahudumu imefutwa au imefanyiwa marekebisho hivyo nafasi yake imeondolewa lakini amechangia kwa muda huo atakuwa na haki ya kupata kiinua mgongo na kusubiri pensheni atakapofikisha umri unaokubalika.


Kukoma uanachama Isipokuwa itakapotangazwa tofauti, mwanachama ambaye uanachama wake unakoma kabla hajafikisha umri wa kustaafu vigezo vya pensheni, kifungu cha 13 cha kanuni hizo kinasema atastahili malipo ya jumla kwa muda aliochangia.

Malipo hayo yatajumuisha michango pamoja na riba ya kila mwaka (compound rate). Fao hili litatolewa kwa wanachama ambao wamefikisha umri wa kustaafu lakini hawajachangia kwa miezi 180 au zaidi.

Kwa ujumla, kiwango cha chini cha pensheni kitakacholipwa kwa mwanachama kitakuwa zaidi ya asilimia 40 ya kima cha chini cha mshahara wa sekta aliyokuwa anafanyia kazi au pensheni anayolipwa mstaafu kabla ya kuanza kutumika kwa kanuni hizi, ikitegemea ipi ni kubwa. “Viwango hivi havitawahusu wanachama watakaojitoa kabla ya kufikisha umri wa kustaafu,” kinasisitiza kifungu cha 14(2) cha kanuni hizo.

Mwanachama akifariki dunia Kwa mwanachama atakayefariki dunia akiwa kazini na kuacha mjane au mgane, mrithi wake atastahili malipo ya asilimia 40 kwa mkupuo na kama wapo zaidi ya mmoja, kiasi hicho kitagawanywa kwa wenza wote huku watoto wake wakipewa asilimia 60. Kama mwanachama hakuwa na watoto, malipo yote atapewa mwenza.

SOURCE: Mwananchi

Post a Comment

0 Comments