Business

header ads

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA VIONGOZI WA TEC, CCT


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo amefanya mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) walioomba kukutana nae na kujitambulisha, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Viongozi wa CCT waliokutana na Mhe. Rais Magufuli ni Mwenyekiti Baba Askofu Anilikisa Cheyo, Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti Baba Askofu Fredrick Shoo, Makamu wa Pili wa Mwenyekiti Baba Askofu Jacob Chimeledya na Katibu Mkuu Mchungaji Moses Matonya.
Viongozi wa TEC waliokutana na Mhe. Rais Magufuli ni Rais Baba Askofu Gervas Nyaisonga, Makamu wa Rais Baba Askofu Flavian Kasalla na Katibu Mkuu Padre Charles Kitima.
Viongozi hao wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukubali ombi lao la kukutana nae kwa lengo la kujitambulisha na kufanya nae mazungumzo kuhusiana na uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Makanisa wanayoyaongoza na Serikali.
Wamemhakikishia Mhe. Rais Magufuli utayari wao wa kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Serikali, kuyasimamia makanisa yao ili yaendelee kutoa huduma ya kiroho na kijamii kwa manufaa ya Watanzania wote na kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Viongozi hao wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta maendeleo na kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya usafiri na majengo, kuleta nidhamu katika utumishi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa, kuimarisha usimamizi wa rasilimali za Taifa hasa madini, kupambana na wizi na ufisadi wa mali za umma, kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, kuimarisha huduma za afya na kuwapigania wakulima.
Wamewaomba Watanzania wote kumpa ushirikiano wa kila aina Mhe. Rais Magufuli kwa kuwa wanatambua na wameona kazi nzuri ambayo anafanya.
Akizungumza baada ya kukutana na viongozi hao Mhe. Rais Magufuli amewashukuru kwa dhamira yao ya kutaka kukutana nae na kufanya nae mazungumzo na amewahakikishia kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa madhehebu ya dini na taasisi zake na itaendelea kushirikiana nayo katika kuwahudumia na kuwaletea maendeleo wananchi.
Mhe. Rais Magufuli ameahidi kufanyia kazi changamoto ambazo madhehebu ya dini yanakutana nazo na amewaomba viongozi hao kuendelea kuliombea Taifa liendelee kudumisha amani, upendo na mshikamano.
Nawahakikishia mimi nipo pamoja na nyinyi, nendeni mkafanye kazi kwa kujiamini na kwa uhuru, mkiwa na jambo lolote nijulisheni nitalishughulikia, wahubirieni Watanzania amani, upendo, mshikamano na kuipenda nchi yao” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Post a Comment

0 Comments