Business

header ads

WASHITAKIWA WATANO KESI YA BILIONEA MSUYA KUNYONGWA HADI KUFAMahakama Kuu ya Tanzania imewahukumu kunyongwa hadi kufa washitakiwa watano baada ya kuwatia hatiani kwa kumuua kwa makusudi mfanyabiashara wa Arusha na Mirerani, Erasto Msuya.


Waliohukumiwa adhabu hiyo ni mshitakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed; mshitakiwa wa tatu, Mussa Mangu; wa tano, Karim Kuhundwa; wa sita Sadick Mohamed na wa saba; Ally Mussa Majeshi.

Hukumu hiyo imetolewa leo Julai 23, 2018 na Jaji Salma Maghimbi aliyesikiliza kesi hiyo.Pia, Mahakama imemwachia huru mshitakiwa wa pili, Shwaibu Jumanne baada ya kukosekana ushahidi dhidi yake.


Awali kesi ya mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara Erasto Msuya, imefikia ukingoni huku upande wa mashtaka ukiegemea mashahidi 32 na vielelezo 26 kujenga msingi wa kesi yao.

Wakati upande wa mashtaka ukiishia mashahidi 32 kati ya 50 waliotarajia kuwaita, utetezi kwa upande wao uliita mashahidi nane na vielelezo vinne kupangua ushahidi wa mashitaka.

Marehemu Msuya alikuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa jijini Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi na bunduki ya kivita ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai.

Katika eneo la tukio, kuliokotwa maganda ya risasi za SMG 22 huku gari ya marehemu aina ya Range Rover T800 CKF, bastola zake na simu zake mbili zikikutwa eneo la tukio.

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, chini ya Jaji Salma Maghimbi aliyesikiliza kesi hiyo, ilipokea vielelezo kadhaa vya kesi hiyo ikiwamo bunduki ya SMG na maganda 25 ya risasi

Pia, ilipokea pikipiki mbili, moja aina King Lion T751 CKB na Toyo 316 CLG zinazodaiwa na mashahidi wa upande wa mashtaka, kuwa zilitumika kusafirisha wauaji.

Mbali na vielelezo hivyo, Mahakama ilipokea vielelezo vya nyaraka ambavyo ni maelezo ya onyo ya kukiri kosa ya washtakiwa watatu na maelezo ya ungamo yaliyotolewa kwa mlinzi wa amani.

Maelezo hayo ya onyo ni ya mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed, mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu, mshtakiwa wa saba, Ally Majeshi na maelezo ya ungamo ni ya mshtakiwa Karim Kihundwa.
Source Mwananchi

Post a Comment

0 Comments