Business

header ads

MAMA SAMIA AKEMEA VITENDO VYA UKATILI KWA WANAWAKE

Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan amelaani na kukemea vikali vitendo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji vinavyoendelea katika jamii na amewataka wananchi kote nchini kushirikiana katika kukabiliana na vitendo hivyo nchini.

Akizungumza mjini Dodoma kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Mh. Samia amesema vitendo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji vinamchukiza sana hivyo ametoa wito maalum kwa wananchi na wadau wote bila kujali dini, kabila wala rangi kupambana ipasavyo na vitendo hivyo ambavyo vinarudisha nyuma jitihada za kumkwamua mwanamke kiuchumi.

Mh. Samia amesema, anafurahishwa na hatua na jitihada zinazochukuliwa na wanawake kote nchini katika kujikwamua kiuchumi kwa kuimarisha shughuli zao za ujasiriamali katika kuelekea uchumi wa viwanda.

Kuhusu uundaji wa majukwaa ya kuwawezesha wanawake kiuchumi nchini, Makamu wa Rais amesema kazi hiyo inaendelea vizuri na kutaka mikoa na wilaya ambazo bado haijaunda majukwaa hayo kufanya hivyo haraka iwezekanavyo.

Amefafanua kwamba, lengo la uundaji wa majukwaa hayo katika ngazi ya wilaya na mikoa nchini ni kuwakutanisha wanawake pamoja katika kujadili na kutafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili ikiwemo tatizo la masoko za bidhaa wanazozizalisha.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake Duniani ni “Tanzania ya Viwanda,Wanawake ni msingi wa mabadiliko ya Kiuchumi”

Post a Comment

0 Comments