Business

header ads

KAMPENI YA NAMTHAMINI YA EATV YAFANIKIWA KUPEKEKA WATOTO 673 SHULENI

 Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki za Wanawake (HAWA) , Joyce Kiria akifafanua jambo kuhusiana na mafanikio makubwa waliyoyapata kupitia kampeni hiyo ya 'NAMTHAMINI'
 Baadhi ya Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo uliofanyika mapema leo jijini Dar.


Kampeni ya kuchangisha fedha za kununulia pedi kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa shule za Sekondari walio katika mazingira magumu nchini iliyokuwa ikiendeshwa na kituo cha East Africa Television (EATV) LTD, kwa ushirikiano na Taasisi ya Hawa imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 20.

Afisa Masoko wa EATV Bi. Basilisa Biseko ametoa takwimu hizo leo Jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari wakati akitoa mrejesho wa kampeni hiyo ya Namthamini, ambayo imefanikiwa kuwaweka shuleni kwa muda wa mwaka mmoja bila ya kukosa masomo wakiwa kwenye siku zao za hedhi wanafunzi wa kike 673.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki za Wanawake (HAWA) Bi. Joyce Kiria amesema kuwa anaishukuru East Africa Television na East Africa Radio kwa kufanikisha kwa hali ya juu zoezi hilo na kusaidia kuongeza ufahamu zaidi kwa umma juu ya tatizo la pedi kwa wanafunzi wa kike.

Katika kampeni hii ambayo wananchi walijitokeza kuichangia katika kuonyesha kumjali mtoto wa kike aliyepo shuleni zilichangwa jumla ya shilingi 20,176,110, ambazo fedha taslim shilingi 11,774,610 na pedi za thamani ya shilingi 8,401,500.

Michango yote ya fedha iliyopatikana itatumika katika kununua pedi na zitaelekezwa moja kwa moja katika shule za Sekondari 20 zenye uhitaji zilizoteuliwa kupata msaada huu, katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Lindi, Pwani na Tanga.

Uongozi wa EATV Limited na Taasisi ya Haki za Wanawake (Hawa Foundation) inapenda kutumia nafasi hii kwa dhati kuwashukuru wananchi wote walioguswa na tatizo la pedi kwa wanafunzi wa kike na kuichangia kampeni ya Namthamini na kuonyesha kuwa kwa pamoja tunaweza. Sisi EATV husema Together Tunawakilisha.

Mwisho kabisa tunapenda kusisitiza kuwa tatizo la wanafunzi wa kike kukosa kuhudhuria shuleni kutokana na kukosa pedi za kujisitiri ni la kwetu sote hivyo East Africa Television Limited pamoja na Taasisi ya Haki za wanawake inatoa wito kwa jamii kuendelea kuungana kwa pamoja katika kusaidia watoto wa kike kupata mahitaji muhimu wawapo shuleni, ili wapate kusoma kwa amani pasipo kukosa kuhudhuria darasani.

Post a Comment

0 Comments