Business

header ads

UNEP WAOMBWA KUKABILIANA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA

Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ameliomba Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, kuisaidia Tanzania kukabiliana na tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini ambao umesababisha mamia ya ekari za misitu kutoweka kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa.

Mh. Samia ametoa ombi hilo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Amesema, pamoja na Serikali kufanya jitihada kubwa za kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira ikiwemo mpango wa upandaji wa miti kote nchini lakini bado msaada na nguvu zaidi unahitajika kutoka shirika hilo ili kuongeza kasi ya kukabiliana na tatizo hilo nchini.

Amesema Tanzania ina mahusiano mazuri na ya muda mrefu na shirika la UNEP ambapo shirika hilo limeweza kuisaidia nchi katika miradi mbalimbali ya kuhifadhi mazingira hivyo mahusiano hayo mazuri ni muhimu yakaja na mbinu bora na nzuri za kuhifadhi mazingira ili kuokoa Taifa lisigeuke jangwa kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa UNEP, Eric Solheim amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira na kusisitiza kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika Uhifadhi wa mazingira nchini.

Post a Comment

0 Comments