Business

header ads

RAIS MAGUFULI , KENYATTA WAZINDUA BARABARA NAIROBI KENYA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta leo wamezindua barabara yenye urefu wa kilometa 28 ya Southern By-pass iliyojengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Nairobi nchini Kenya.

Akizungumza katika sherehe hiyo ilifanyika katika eneo la Karen nje kidogo ya Jiji la Nairobi, Rais Magufuli amempongeza Rais Kenyatta na Serikali yake kwa kujenga barabara hiyo ambayo sio tu itawasaidia wananchi wa Kenya bali pia itawasaidia wananchi wa Afrika Mashariki wanaotumia barabara zinazopitia Nairobi.

Rais Magufuli pia ameishukuru Serikali ya China kupitia benki yake ya Exim ambayo imetoa mkopo wa kujenga barabara hiyo, kwa kuendelea kuziamini nchi za Afrika Mashariki na kuzikopesha mikopo inayosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara.

Kwa upande wake Rais Kenyatta amesema kujengwa kwa barabara hiyo kumesaidia kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Nairobi na pia kutaboresha shughuli za maendeleo ya wananchi.

Mhe. Kenyatta amemshukuru Rais Magufuli kwa kuungana nae kuzindua barabara hiyo na amesema Kenya itaongeza juhudi katika utekelezaji mradi wa ujenzi wa barabara zinazounganisha Kenya na Tanzania zikiwemo barabara ya Malindi kupitia Saadani hadi Bagamoyo nchini Tanzania na barabara ya Voi - Taveta- Horiri-Arusha.

Kabla ya kuzindua barabara hiyo Rais Magufuli ametembelea kiwanda kidogo cha kusindika maziwa cha Eldoville kilichopo katika eneo la Karen ambacho kinamilikiwa na familia ya mkulima Bw. James Karuga.

Post a Comment

0 Comments