Business

header ads

WABUNIFU MAJENZI KUPEWA KIPAUMBELE MIRADI YA NDANIWaziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kuungana ili waweze kupata fursa katika miradi mikubwa ya ujenzi inayotarajiwa kuanza hivi karibuni nchini Tanzania.

Prof. Mbarawa alisema hayo wakati wa ufunguzi wa semina endelevu ya 26 ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, ambapo amesema Serikali ya Awamu ya Tano itatoa kipaumbele kwa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi watakaoungana ili kuwa na nguvu ya kutekeleza miradi hiyo kwa viwango vyenye ubora.

Akitaja baadhi ya miradi hiyo Prof. Mbarawa amesema kuwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa miundombinu ya kisasa mjini Dodoma, ujenzi wa makazi ya kisasa ya wananchi, vyote hivyo kuungana kwa wataalamu hao kutaongeza nguvu ya kufanya kazi kwa haraka na ubora unaokubalika.
Aidha ameitaka Bodi ya Usajili ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), kujitangaza na kuwatangaza wataalamu wake ili huduma zao zitumiwe na wananchi wa ngazi zote kwa gharama nafuu.
Shirikianeni na vyuo vinavyofundisha fani yenu ili viongeze udahili wa wanafunzi na kuhakikisha kazi zenu zinafanywa kisasa na kwa kuzingatia teknolojia”, amesema Prof. Mbarawa.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya AQRB, Mbunifu Majengo Ambwene Mwakyusa, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Bodi yake imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata ramani za nyumba kwa bei nafuu ili kuwa na jamii yenye makazi ya kisasa.

Naye Msajili wa Bodi ya AQRB, Mbunifu Majengo Jehad Jehad amesema takribani Wabunifu majengo na Wakadiriaji majenzi 1,333 pamoja na kampuni za fani hiyo 372 zimesajiliwa na zinatoa huduma kwa mujibu wa sheria za fani hiyo.

Bw. Jehad alisema kuwa Bodi yake imejipanga kuhakikisha maadili ya taaluma hiyo hapa nchini yanalindwa na atakayekiuka atafutiwa usajili na kuadhibiwa kwa mujibu wa taratibu ya bodi hiyo.

Zaidi ya miradi ya ujenzi 1,963 imekaguliwa na bodi hiyo katika maeneo mbalimbali nchini katika kipindi cha mwaka wa 2015 lengo ikiwa ni kuhakikisha ujenzi wowote unaofanyika nchini unakuwa na viwango bora.


Post a Comment

0 Comments