Business

header ads

WANAFUNZI 290 HAWANA SIFA UDOM


Na: Lilian Lundo

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa wanafunzi 290 kati ya wanafunzi 7,805 wa Stashahada Maalum ya Ualimu Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) waliorejeshwa nyumbani Mei, 2016 kutokana na mgomo wa walimu katika chuo hiko hawakuwa na sifa ya kujiunga na programu hiyo.

Prof. Ndalichako aliyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu maamuzi yaliyochukuliwa na Serikali baada ya kugundulika kudahiliwa kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa katika programu hiyo.

“Programu hii ilikuwa maalumu kwa ajili ya kutatua tatizo la upungufu wa walimu wa sayansi nchini, ambapo wanafunzi waliotakiwa kujiunga na programu hii ni wale waliomaliza kidato cha nne na wamefaulu  Daraja la I hadi la III na kupata  alama C au zaidi kwa masomo mawili ya Sayansi na Hisabati,” alifafanua Prof. Ndalichako.

Aliendelea kwa kusema kuwa, kati ya wanafunzi 290 wasiokuwa na sifa wapo ambao walidahiliwa pasipokuwa na alama C au zaidi katika  masomo ya sayansi na hisabati na wengine ambao walifaulu kwa Daraja la IV kinyume na Sifa zilizotolewa.

Aidha, Mhe. Ndalichako amesema kuwa programu hiyo ilikuwa maalumu kwa ajili ya walimu wa Sekondari ili kutatua tatizo la uhaba wa walimu wa Sayansi na Hisabati katika shule za Sekondari lakini kuna wanafunzi 1,210 waliokuwa wakisoma Stashahada ya Ualimu wa shule ya Msingi kinyume cha matakwa ya programu hiyo.

Hivyo basi, Serikali imewarejesha wanafunzi 382 kuendelea na masomo yao chuo kikuu cha UDOM, wanafunzi wengine 4,586 watahamishiwa vyuo vya ualimu Morogoro, Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu pamoja na wanafunzi 1,337 ambao watahamishiwa kwenye vyuo vya Ualimu Korogwe na Kasulu.

Aidha, wanafunzi 290 waliokosa sifa wameshauriwa kuomba mafunzo yanayolingana na sifa walizonazo kwenye vyuo watakavyotaka na wale waliokuwa wakisomea Ualimu shule ya Msingi 29 watahamishiwa chuo cha Ualimu Kasulu kumalizi masomo kwa gharama zao na wanafunzi 1,181 wametakiwa kuomba mafunzo yanayolingana na sifa walizonazo.

Hata hivyo, Serikali itaendelea kuwapatia mikopo wanafunzi watakaorejeshwa UDOM na watakaohamishwa kwenye vyuo vya Ualimu vya Serikali watapewa mkopo wa kiasi cha Sh. 600,000 kwa mwaka ambayo ni ada ya mafunzo ya Ualimu itakayolipwa moja kwa moja chuoni.

Prof. Ndalichako amesema kuwa mgomo wa walimu wa chuo cha UDOM umetokana na wingi  wa wanafunzi waliodahiliwa kwa ajili ya stashahada maalumu ya ualimu ambapo wanafunzi 7,845 walidahiliwa huku chuo kikiwa na uwezo wa kuwa na wanafunzi 1,080.

Walimu hao, walikuwa wakifundisha wanafunzi wa stashahada ya ualimu na wanafunzi wa Shahada wa chuoni hapo hali iliyopelekea walimu hao kuzidiwa wakati huo huo, uongozi wa chuo haukuwa ukitoa fedha za ziada kwa walimu hao, hivyo kupelekea kugoma kutokana na changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo.


Post a Comment

0 Comments