Business

header ads

VIONGOZI WA AFRIKA WAASWA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAJIWaziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akiongea na wajumbe wakati wa Ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita wa Wiki ya Maji ya Afrika, ambapo aliwaasa kujadili na kuona namna bora ya kuwapatia majisafi na salama wananchi waishio vijijini, leo Jijini Dar es Salaam.

 Mwakilishi maalum wa Masuala ya Maji kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Rais Mstaafu wa Kenya Mhe. Mwai Kibaki akiongea na wajumbe wakati wa Ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita wa Wiki ya Maji ya Afrika, ambapo aliwataka wadau katika Sekta ya Maji kushiriki katika kutatua changamoto za upatikanaji wa Maji katika nchi zao leo Jijini Dar es Salaam.

Rais wa AMCOW ambaye pia ni Waziri wa Maji kutoka Senegal Amodou Mansour Faye akiongea na wajumbe wakati wa Ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita wa Wiki ya Maji ya Afrika, ambapo alisema kuwa wajumbe wanawajibu wa kujadili na kubadilishana uzoefu wakati wa mkutano na baada ya mkutano kwa manufaa ya wananchi wa nchi wanazoziwakilisha.

 Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge akiongea na wajumbe wakati wa Ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita wa Wiki ya Maji ya Afrika, ambapo amesema kuwa malengo ya Tanzania ni kuhakikisha kufikia mwaka 2020, Serikali imedhamiria kufikisha maji katika maeneo yote nchini ambapo kwa upande wa vijijini inatarajiwa kufikia asilimia 85 na asilimia 95 kwa upande wa mijini.

  Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwakilishi maalum wa Masuala ya Maji kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Rais Mstaafu wa Kenya Mhe. Mwai Kibaki wakati wa Ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita wa Wiki ya Maji ya Afrika,Katikati ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge leo Jijini Dar es Salaam.


 Wajumbe waliohudhuria Ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita wa Wiki ya Maji ya Afrika, wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, leo Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge (kushoto) akiwaongoza  wajumbe wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Nchi za Afrika Katibu wa Mtendaji wa AMCOW Bw. Bai-Mass Taal (katikati) na Rais wa AMCOW Bw. Amodou Mansour Faye kutembelea Mabanda ya wadau wa Sekta ya Maji waliohudhuria Maadhimisho ya Sita wa Wiki ya Maji ya Afrika, leo Jijini Dar es Salaam.


PICHA NA HASSAN SILAYO


Na Eleuteri Mangi

Viongozi wanaoshiriki Ufunguzi wa Maadhimisho ya Sita wa Wiki ya Maji ya Afrika, na Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa Maji barani Afrika (AMCOW) wameaswa kujadili na kuona namna bora ya kuwapatia majisafi na salama wananchi waishio vijijini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokuwa akifungua maadhimisho hayo  yanayoshirikisha wadau wa maji barani Afrika na ulimwenguni kwa ujumla leo jijini Dar es Salaam.

“Wananchi waliopo vijijini bado wana uhitaji mkubwa wa maji, kwa kupitia mkutano huu mawaziri wa maji, wataalamu wa sera na wadau wa maendeleo mkae pamoja, muone namna sahihi ya kuwapatia watu maji” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa, kupitia mkutano huo wajumbe watajadiliana na kubadilishana uzoefu ambapo Tanzania itanufaika kwa kuwa ina neema kubwa ya vyazo vingi vya maji ikiwemo bahari, maziwa pamoja na mito, ambayo ni muhimu katika upatikanaji wa maji kwa watanzania na nchi jirani.

Akitolea mfano, Waziri Mkuu alisema kuwa kupitia Ziwa Victoria, Tanzania inapakana na nchi za Uganda na Kenya, Ziwa Nyasa na Malawi pamoja na Msumbiji, na Ziwa Tanganyika Tanzania inapakana na Zambia pamoja na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, ambapo vyanzo hivyo vya maji vinaweza kutumika kuwahudumia watu wa maeneo hayo kwa manufaa ya maendeleo ya sekta mbalimbali.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza kuwa wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji wavitunze ili wananchi wanaotegemea vyanzo hivyo waendelee kupata huduma ya maji endelevu kwa matumizi mbalimbali.

Akizunguzia namna Tanzania inavyoshiriki mkutano huo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema kuwa malengo ya Tanzania ni kuhakikisha kufikia mwaka 2020, Serikali imedhamiria kufikisha maji katika maeneo yote nchini ambapo kwa upande wa vijijini inatarajiwa kufikia asilimia 85 na asilimia 95 kwa upande wa mijini.

Waziri Lwenge ameongeza Serikali imejipanga na kuipa Sekta ya Maji kipaumbele, ambapo katika bajeti ya mwaka huu zimetengwa zaidi ya Sh. trilioni 1 na hadi kufikia 2030 Tanzania itakuwa imekamilisha miradi yote ya maji kwa asilimia 100. Hayo yakiwa ni malengo ya nchi za Afrika ya kuwapatia wananchi wote mijini na vijijini maji kwa asilimia 100 hadi kufikia mwaka 2030.

Akiwakaribisha wageni waalikwa kwenye mkutano huo Rais wa AMCOW ambaye pia ni Waziri wa Maji kutoka Senegal Amodou Mansour Faye alisema kuwa wajumbe wanawajibu wa kujadili na kubadilishana uzoefu wakati wa mkutano na baada ya mkutano kwa manufaa ya wananchi wa nchi wanazoziwakilisha.

Maadhimisho ya Wiki ya Maji ya Afrika pamoja na Mkutano wa AMCOW unafanyika nchini kwa mara ya kwanza yanaongozwa na kauli mbiu ya “Kufikia lengo la maendelevu (SDGs) juu ya usalama wa maji na usafi wa Mazingira”.

Kwa mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwake maadhimisho ya Wiki ya Maji ya Barani Afrika na Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Maji barani Afrika yalifanyika nchini Tunisia mwaka 2008 katika mji wa Tunis, 2009 ulifanyika Mindrad Afrika ya Kusini, mwaka 2010 Adids Ababa nchini Ethiopia, mwaka 2012 Cairo nchini Misri  na mwaka 2014 mkutano huo ulifanyika 2014 Dakar Senegal.

Post a Comment

0 Comments