Business

header ads

TAARIFA YA UNICEF KUHUSU SIKU YA WATOTO NJITI DUNIANI

Nchini Tanzania, kila mwaka, watoto takribani 213,000 huzaliwa mapema sana kabla ya muda wao (watoto njiti) na zaidi ya 9,000 miongoni mwao hufariki kutokana na matatizo yanayohusiana na kuzaliwa mapema mno. Idadi hii ni takribani robo ya watoto wachanga 40,000 wanaofariki kila mwaka hapa nchini. Vifo kutokana na matatizo yanayohusiana na kuzaliwa kabla ya muda kutimia ni sababu kubwa ya pili inayosababisha vifo vya watoto wachanga hapa Tanzania.


Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya watoto. Vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 166 kati ya 1,000 waliozaliwa hai mwaka 1990 hadi kufikia vifo 54 kati ya kila 1,000 waliozaliwa hai mwaka 2012. Hata hivyo kasi ya kupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa mwezi mmoja imekuwa ndogo, kutoka watoto 43 kati ya 1,000 waliozaliwa hai mwaka 1990 hadi watoto 21 kati ya 1,000 waliozaliwa hai mwaka 2012. Pia kasi ya kupunguza vifo vya watoto wachanga vinavyotokana na matatizo ya kuzaliwa njiti ni ndogo sana na hivyo basi vinaendelea kuchangia asilimia kubwa ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Kila siku zaidi ya watoto wachanga 100 hufariki nchini Tanzania, kutokana na maambukizi, matatizo yanayojitokeza wakati wa kuzaliwa kama vile kupumua kwa shida na matatizo yanayotokana na kuzaliwa kabla ya muda (watoto njiti). Nchini Tanzania, vifo vya watoto wachanga vinachangia hadi asilimia 40 ya vifo vyote vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Kimsingi, vingi kati ya vifo hivi vya watoto wachanga vinaweza kuepukika kwa kutumia huduma za gharama nafuu zenye ufanisi. Takwimu hizi zinaonesha haja ya kuwa makini zaidi na kuchukua hatua madhubuti kwa ajili ya watoto wachanga na mama zao. Kwa mujibu wa Mpango Kazi wa Kila Mtoto Mchanga (Every Newborn Action Plan) ambao ni mpango kazi wa kimataifa wa kutokomeza vifo vinavyoweza kuepukika, kipindi muhimu cha kuokoa maisha ya maelfu ya akina mama na watoto wachanga ni wakati wa kuzaliwa na ndani ya masaa 24 ya kwanza ya maisha ya mtoto mchanga, kwani kipindi hicho ndipo asilimia 40 ya watoto wanazaliwa wakiwa wameshafariki (uzazimfu) na vifo vya watoto wachanga; na asilimia 48 ya vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi hutokea

Mwaka huu 2014, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikiwa imeungwa mkono na na wadau mbalimbali, imeanzisha mpango mkakati (Sharpened One Plan) wa Kuharakisha zaidi Kupunguza Vifo vya akina Mama vinavyotakana na uzazi, pamoja na vifo Watoto Wachanga na vya Watoto wenye umri Chini ya miaka mitano, Tanzania mwaka 2014-15. Mpango huu umeweka kipaumbele dhamira ya kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya watoto wachanga na vya akina mama vinavyotokana na uzazi hususan kufatilia kwa kina suala la uzazi wa mpango, huduma za afya wakati wa kujifungua na uwepo wa dawa muhimu ili kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika. Iwapo mpango huu ukitekelezwa nchi nzima, tutaweza kuokoa maisha ya akina mama 1,400, watoto wachanga 9,400 na kupunguza vifo 2500 vya watoto wanaozaliwa wakiwa wamefariki (uzazimfu) ifikapo mwaka 2015.

Watoto njiti wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kufariki na kupata ulemavu
Watoto wanaozaliwa kabla ya muda wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kufa kutokana na magonjwa ya mfumo wa hewa, mfumo wa chakula na mfumo wa fahamu ukilinganisha na watoto waliozaliwa baada ya kutimiza wiki 37 au zaidi wakiwa tumboni mwa mama zao. Watoto njiti pia wapo katika hatari ya kupata matatizo ya kuona, kusikia, kutambua/kiakili na moyo yanayoweza kudumu maisha yao yote. Zaidi ya hapo watoto wanaozaliwa njiti katika nchi zilizo na uchumi duni wapo katika hatari ya kufa mara 10 zaidi ukilinganisha na watoto njiti wanaozaliwa katika nchi zilizoendelea.

Tunaweza kupunguza idadi ya njiti
Sababu kuu zinazosababisha hali ya hatari kwa watoto njiti nchini Tanzania na nchi nyingine zenye uchumi mdogo ni maambukizi wakati wa ujauzito, malaria, VVU, kuzaliwa na uzito mdogo, muda mfupi kati ya uzao mmoja na mwingine na mimba za utotoni. Matunzo sahihi kabla, katikati na wakati wa ujauzito (ikiwemo uzazi wa mpango na huduma wakati wa ujauzito) ni muhimu katika kupunguza kiwango cha uzazi wa watoto njiti. Hata hivyo sehemu kubwa ya sababu zinazofanya watoto kuzaliwa njiti hazijulikani. Hivyo basi tunahitaji kufanyike tafiti zaidi ili kupata uelewa na kudhibiti visababishi vyake.

Tunaweza kupunguza vifo vya watoto wachanga wanaokufa kutokana na matatizo ya kuzaliwa njiti
Mtoto anayezaliwa njiti sio lazima apewe uangalizi wa karibu (intensive care) na kutumia teknolojia kubwa sana ili aishi. Huduma za gharama nafuu zinazoweza kufanyika ili kuongeza uwezekano wa mtoto mchanga kuishi na kupunguza hatari kwake ya kupata ulemavu wa maisha, ni pamoja na zifuatazo:

Antenatal steroids, hizi ni dawa ambazo hutolewa kwa akina mama wanapopata uchungu wa kujifungua kabla ya wakati, katika ngazi za afya zinazostahili, husaiidia kukuza mapafu ambayo hayajakomaa ya mtoto njiti na kuzuia matatizo kwenye mfumo wa hewa ya watoto wachanga.
Huduma ya Mama Kangaruu: Hii ni mbinu ya kumbeba mtoto mchanga kwenye kifua cha mama yake wakigusana ngozi kwa ngozi ili kumpa joto na kurahisisha unyonyeshaji. Ni muhimu kuwapatia joto watoto njiti kwa sababu miili yao ni midogo na hupoteza joto haraka, jambo linalowafanya kuwa kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa mbalimbali, maambukizi na kifo. Inakadiriwa kuwa mbinu hii ya Mama Kangaruu inaweza kuepusha vifo vya watoto 5,000 kila mwaka hapa Tanzania.
Kusaidia watoto kupumua kwa kutumia bag na mask ni huduma muhimu kwa watoto njiti wenye matatizo ya kupumua. Iwapo huduma hii rahisi ya kusaidia watoto wachanga kupumua inapatikana kwa asilimia 90 ya watoto wanayoihitaji, basi takribani maisha ya watoto wachanga 2,000 yangeweza kuokolewa kila mwaka. Mpango wa Kusaidia Watoto Kupumua (Helping Babies Breathe) ulizinduliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii mwaka 2009 kwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa sekta ya afya katika ngazi zote, ukiwa na lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga vinavyotokana na matatizo ya kupumua. Wadau wa afya mbalimbali wameshirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kutekeleza mpango huu.
Kumsaidia mama kuanza kunyonyesha mtoto ndani ya saa moja baada ya kujifungua, hii inahusisha pia kumsaidia mama kukamua maziwa kwa ajili ya mtoto na kumpa kwa kutumia kikombe pale inapo lazimu.
Kuzuia, kutambua mapema na kutibu maambukizi: utoaji wa huduma inayozingatia usafi wakati wa mama kujifungua (mfano kuosha mikono, uhudumiaji sahihi wa kitovu na ngozi ya mtoto mchanga) ni muhimu katika kuzuia maambukizi kwa mama na mtoto. Dawa za antibiotiki kama vile Amoxicillin zinaweza kutumiwa kutibu nimonia na Gentamicin kwa ajili ya kutibu maambukizi makubwa yanayowapata watoto wachanga.

Zaidi ya hapo, watoto wote wachanga wanahitaji kukaguliwa afya zao ndani ya masaa 24 na baada ya siku 3 ya kuzaliwa ili kuzuia matatizo yanayoweza kutokea na yale ambayo yanaweza kusababisha ulemavu katika maisha yao ya baadaye.

Huduma bora inahitajika wakati wa kujifungua na hususan kwa watoto wachanga wanaozaliwa na uzito mdogo na wale walio wagonjwa.
“Watoto wachanga wanahitaji kupata huduma muhimu hususan kwa wale ambao wanazaliwa kabla ya muda wao,” anasema Mwakilishi wa Unicef nchini Tanzania Dk. Jama Gulaid. “Hii inajumuisha kuwakausha, kuwapa joto na kuwaweka safi, kuwaanzisha kunyonya ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa na kuhakikisha kwamba watoto wanaopata shida kupumua wanapata huduma na uangalizi wa haraka. Dakika ya kwanza baada ya kuzaliwa ni dakika ya dhahabu (golden minute) kwa kila mtoto mchanga.”

Kuna ushahidi wa uhakika kwamba utolewaji wa huduma muhimu wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua bila ya kutumia gharama kubwa na uangalizi wa karibu (intensive care) unaohitaji teknolojia ya juu, unaweza kuokoa maisha ya watoto wengi wanaozaliwa kabla ya muda na wengi wao wakaweza kukua na kuwa na afya nzuri bila ya ulemavu wa kudumu.

Kama ilivyoainishwa katika Mpango Kazi wa Kila Mtoto Mchanga (Every Newborn Action Plan) na Mpango mkakakati wa kuharakisha zaidi kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi, pamoja na vifo vya watoto wachanga na vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano (Sharpened One Plan) tunahitaji kuimarisha na kuwekeza zaidi kwenye huduma wakati wa kujifungua na katika wiki ya kwanza ya maisha ya mtoto. Uboreshaji huduma za akina mama wajawazito na watoto wachanga zinazotolewa katika vituo vya afya na katika jamii, vitapunguza tofauti na kuleta usawa katika jamii kwa kuhakikisha kila mama na mtoto mchanga wanafikiwa na huduma; kutumia nguvu za wazazi, familia na jamii; na kumhesabu kila mtoto mchanga kwa kutumia vipimo maalumu, uwepo wa mipango ya ufuatiliaji wa programu na uwajibikaji, duniani kote pamoja na Tanzania. Kila mwananchi ana mchango wake katika kudai huduma bora na kuwekeza kwenye afya.

“Jambo moja muhimu, tunahitaji kuwaongezea mafunzo na kuwaunga mkono wale wote wanaotoa huduma za kuzalisha na huduma kwa watoto wachanga kuanzia madaktari bingwa wa akina mama, madaktari bingwa wa watoto, madaktari, wakunga na wauguzi,” anasema Dk. Jama Gulaid.

Wadau mbalimbali pamoja na UNICEF wanaunga mkono juhudi za Wizara za Afya katika kutathmini hali ya watoto wachanga, kuainisha changamoto na njia kuu za kuzikabili ili kuboresha afya ya mtoto mchanga Tanzania bara na visiwani. Wadau wapo tayari kuisaidia serikali kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ili watoe huduma bora kwa akina mama wajawazito, watoto wachanga na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ikiwemo Kusaidia watoto wachanga kupumua, huduma ya Mama Kangaroo, huduma za Dharura wakati wa Ujauzito, huduma Muhimu kwa Watoto Wachanga, pamoja na kutoa vifaa na zana muhimu na kujenga uelewa na hamasa katika jamii ya kudai na kutumia huduma bora za afya za mama na mtoto.

Wadau wamekuja pamoja kuadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani na kurudia ahadi waliyotoa ya kutokomeza vifo vya watoto ambavyo vinaepukika. Kuboresha afya ya watoto wachanga pamoja na kuzuia watoto kuzaliwa njiti na kuhakikisha utolewaji wa huduma bora kwa mtoto mchanga ni sehemu muhimu ya harakati hii.

Post a Comment

0 Comments