Business

header ads

MWINYI ASISITIZA MATUMIZI YA KISWAHILI MASOMO YA SAYANSI

Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amewataka walimu wa shule za sekondari nchini kuwafundisha wanafunzi wao masomo ya sayansi kwa lugha ya Kiswahili, ili kukuza na kuongeza idadi ya wanasayansi watakaoliletea sifa taifa.Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akitoa tuzo kwa wanafuzi wa shule za sekondari nchini waliofanya vizuri katika ugunduzi na tafiti mbalimbali za kisayansi walizozifanya, lengo likiwa ni kuimarisha taaluma hiyo pamoja na kutoa hamasa ya kusoma masomo ya sayansi.

Alisema masomo ya sayansi yanaweza kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili na wanafunzi wakaelewa vizuri kuliko kutumia lugha ya kiingereza.

Alisema kuna nchi nyingi duniani zinatumia lugha zao kufundishia masomo ya sayansi darasani na wanafunzi wanaelewa na wanakuwa wanasayansi wakubwa.

“ Masomo ya sayansi yanaweza kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili, hivyo walimu msiogope kwa kuwa mtahamasisha wanafunzi wengi kupenda kujifunza masomo ya sayansi,” alisema Mwinyi.

Aliongeza kuwa hata yeye wakati anasoma sekondari alikuwa anafundishwa masomo ya sayansi na mwalimu kutoka nchi ya Scotland na alikuwa anaelewa vizuri masomo hayo.

Alisema sababu kubwa inayowafanya wanafunzi wa sekondari kukimbilia mchepuo wa sanaa ni uwepesi wa masomo hayo wa kutokuwa na maneno magumu kuliko masomo ya sayansi.

Maonesho hayo yaliandaliwa na Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi (YST) huku wanafunzi kutoka sekondari ya Mzumbe ya mkoani Morogoro waliibuka washindi wa jumla na kuzawadiwa udhamini wa kusoma masomo ya vyuo vikuu pamoja na kutembelea nchi ya Ireland.

Katika utafiti wao, wanafunzi hao walieleza jinsi ambavyo mifuko ya plastiki inavyoleta athari kwa jamii, mazingira na mifugo pia wakiiasa jamii kutotumia bidhaa hiyo.

Maonesho hayo yaliwashirikisha wanafunzi takribani 240 wa sekondari na walimu 120 wakionesha kazi mbalimbali za kisayansi.

Makamu wa Rais wa kampuni ya uchimbaji mafuta na gesi (BG), John Ulanga ambao ndiyo wadhamini alisema mwaka huu wametoa wametoa dola za Marekani 200,000.

Naye Mkurugenzi wa YST,Dk. Gozibert Kamugisha amesema nchini kuwa wanafunzi wengi wa sekondari wanavipaji vya kufanya utafiti lakini wameshindwa kujiendeleza kutokana na kukosa msaada.

Kwa upande wao wanafunzi walioshiriki mashindano hayo wameitaka serikali ya Tanzania imetakiwa kufanya jitihada za kukuza lugha ya Kiswahili kwa kuweka kipaumbele katika ufundishaji katika shule za sekondari ili wanafunzi wengi zaidi wajiunge na vyuo vya elimu ya juu na kusomea Kiswahili ili kupata fursa ya ajira katika nchi mbalimbali duniani kupitia lugha ya Kiswahili.

Wanafunzi hao wa Shule za Sekondari wamesema iwekwe sera madhubuti ya kuhamasisha wanafunzi pamoja na wananchi kwa ujumla kufahamu fursa za kielimu na kiuchumi zinazopatikana kupitia lugha ya Kiswahili..

Post a Comment

0 Comments