Business

header ads

CHADEMA WATAJA MAJIMBO WATAYOSIMAMISHA WAGOMBEA WAO


  Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, akizungumza katika mkutano huo.
 Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi,  Nderakindo Kessy (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho, Ilala Dar es Salaam jana, wakati akitangaza majimbo yaliyochini ya vyama vinavyounda Ukawa ambayo vyama hivyo vitasimamisha wagombea wao katika uchaguzi mkuu. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Masudi Makunjunga.
 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza majina ya wagombea ubunge katika majimbo 135 yaliyoteuliwa na Kamati Kuu yakiwamo ya wabunge na makada wa CCM waliohamia katika chama hicho.
Taarifa iliyotolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Bara, John Mnyika iliorodhesha majina ya wagombea wote na majimbo yao isipokuwa 12 ambayo hayajafikiwa maafikiano ndani ya Ukawa.
Katika orodha hiyo wamo baadhi ya waliokuwa wabunge na makada wa CCM, Ester Bulaya aliyeteuliwa kugombea Bunda Mjini, James Lembeli (Kahama Mjini) na Said Nkumba (Sikonge).
Pia, katika orodha hiyo ambayo imechapishwa katika Ukurasa wa 35 wa gazeti hili, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole ameteuliwa kugombea ubunge jimbo la Longido kwa tiketi ya Chadema.
Vilevile, kada wa Chadema, Fred Mpendazoe ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Kishapu kwa tiketi ya CCM, atagombea katika jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema baada ya kulikimbia Jimbo la Segerea alilogombea mwaka 2010 na kuangushwa na Dk Makongoro Mahanga ambaye naye amejiunga na Chadema hivi karibuni.
Orodha hiyo pia inajumuisha jina la Naibu Waziri wa zamani wa Kilimo, Njelu Kasaka aliyehamia Chadema, kugombea katika jimbo la Lupa. Baadhi ya wagombea ambao walishindwa kwenye kura za maoni na kurudishwa na Kamati Kuu ni pamoja na Mwita Waitara (Ukonga) na Ansbert Ngurumo (Muleba Kaskazini).
Mgawanyo wa majimbo balaa
Wakati huohuo; mgawanyo ya majimbo chini ya Ukawa na uamuzi wa Chadema kuwarejesha baadhi ya wagombea ubunge walioshindwa katika kura ya maoni ulizua sintofahamu katika maeneo kadhaa.
Hali hiyo siku moja baada ya Ukawa kutangaza mgawanyo wa majimbo na Chadema kupata 138, CUF 99, NCCR 14 na NLD matatu.
Pamoja na mgawanyo huo ulioelezwa kufanyika baada ya kuafikiana, hali ya sintofahamu iliibuka katika jimbo la Mbarali mkoani Mbeya baada ya makada wa Chadema na CUF kuchukua fomu za kugombea ubunge, kinyume na uamuzi wa kusimamisha mgombea mmoja. Maeneo mengine yanayotajwa kuwa na mvutano mkali kuhusu mgawanyo wa majimbo ni Solwa, Singida Mjini, Kilombero na Kibaha.
“Kuna baadhi ya majimbo makada wa Chadema wamekilalamikia chama hicho wakidai kuwa kina nguvu zaidi, hivyo kitendo cha kuachia majimbo hayo kupewa vyama vingine vinavyounda Ukawa ni sawa na kuyapoteza kwa sababu ya vyama hivyo kutokuwa na mtandao na kuwa na wagombea wasio na nguvu,” kilieleza chanzo cha habari hizo. Hata hivyo, chanzo hicho kilisema majadiliano yalikuwa yanafanyika.
Mbarali
Katika Jimbo la Mbarali, mgombea wa Chadema Liberatus Mwang’ombe alichukua fomu za ubunge katika Ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi na kuungana na Gamdusti Juma Haji (CUF) aliyechukua fomu hizo Agosti 15.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wenyeviti wa wilaya wa vyama hivyo, walisema kila chama kimefikia uamuzi huo baada ya kutokubaliana kuachiana jimbo hilo.
Mwenyekiti wa Chadema Mbarali, Peter Mwashiti alisema walifikia uamuzi wa kumruhusu Mwang’ombe kuchukua fomu hiyo kutokana na kushindwa kuelewana baina yao na wenzao wa CUF.
Alisema awali walipewa taarifa kwamba kamati kuu ya Ukawa iliamua jimbo hilo lichukuliwe na CUF lakini wao (Chadema wilaya) wakapeleka vielelezo kwamba mgombea aliyependezwa na CUF pamoja na chama chenyewe hawana nguvu ya kushindana na CCM.
“Wakati tunaendelea na vikao vyetu, tukasikia mgombea wa CUF amechukua fomu, hivyo na sisi tumeamua mgombea wetu akachukue fomu wakati tunaendelea na vikao,” alisema Mwashiti.
Mwenyekiti wa CUF wa wilaya hiyo, Bob Magagula alisema walifikia uamuzi huo baada ya kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa viongozi wa vyama hivyo ngazi ya wilaya.
“Chadema hawamuamini kabisa mgombea wetu, wakati sisi CUF tunamkubali… na sababu kubwa eti mgombea wetu anatumika na mgombea wa CCM kwa vile tu ni ndugu japo kuna ukweli kwamba hawa jamaa ni ndugu lakini hii si sababu ya kumkataa,” alisema.
Moshi Vijijini
Mkoani Kilimanjaro, wanachama watatu wa Chadema akiwamo Katibu wa Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema jana walijeruhiwa baada kupigwa na vijana wa ulinzi wa chama hicho katika mzozo wa kurudiwa kura za maoni Katika vurugu hizo zilizotokea jana, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu anadaiwa kuchomoa bastola yake kabla ya kuzuiwa na ofisa usalama wa Chadema, Allan Bujo.

Post a Comment

0 Comments