Business

header ads

RIPOTI YA WALIOTAMBULIWA AJALI MAFINGA IRINGA
MIILI nane tu kati ya 43 ya marehemu waliofariki katika ajali ya juzi iliyohusisha basi na roli katika eneo la Changarawe, Mafinga mkoani Iringa ndio iliyotambuliwa mpaka leo mchana.

Idadi ya marehemu wa ajali hiyo iliongezeka kutoka 42 waliofariki mapema juzi hadi 43, baada ya majeruhi aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Iringa, Oswald Mwinuka (58) kukata roho usiku wa kuamkia jana.

Wakati taarifa ya awali kutoka vyanzo mbalimbali ilidai wengi waliofariki katika ajali hiyo walikuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi inaonesha wanaoendelea kutambuliwa walikuwa wafanyabishara wa eneo la Soweto, mjini Mbeya.

Alisema imekuwa ngumu kutaja majina ya watu wote waliofariki kwakuwa hawajatambuliwa na kuthibitishwa na ndugu zao.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Robert Salim alisema kati ya maiti 27 zilizofikishwa hospitalini hapo juzi kutoka Mafinga ni nane tu zilizotambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao wengi wao kutoka jijini Mbeya.

Mbali na Mwinuka, Kamanda Mungi alitaja miili iliyotambulikuwa kuwa ni Mbezi Deogratius  (29), Editha Ngunangwa (28), Mohamed Juma (32) na Ndenya Sixbert (25) ambao wote walikuwa wakazi wa Soweto Mbeya.

Wengine ni James Kinyamaguho (30) mkazi wa Morogoro, Said Halfan (35) na Abuu Mangula (35) ambao pia ni wakazi wa Mbeya.

Aliwataja waliojeruhiwa ambao wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Iringa na ya wilaya ya Mufindi ya Mafinga kuwa ni Mustafa Ally, Dominic Shauri, Tito Kyando, Martin Haule, Ipyana Mbamba, Fadhil Kalenga, Mussa Mwasege, Nehemia Mbuji, Josam Abel, Tumpate Mwakapala, Nico Hamis na Ester William.

Wengine ni Peter Mwakanale, Kelvin Mwakaladi, Raphael Nerbot, Maga Sebastian, Catherine Mwijungu, Lucy Mtanga, Debora Vicent, Ester na mwanaume ambaye jina lake halijaweza kujulikana kutokana na kuwa na hali mbaya.


Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Salim alisema hali za majeruhi wanne waliolazwa Hospitali ya rufaa ya Iringa inaendelea vizuri wakati wengine wanne hali zao sio nzuri na wanatarajia kuwapa rufaa kwenda hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
SOURCE BONGO LEAKS


Post a Comment

0 Comments