Business

header ads

WANAFUNZI 84 UDOM WATIWA MBARONI Wanafunzi 84 wa Chuo Kikuu UDOM wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuhamasisha uvunjifu wa amani chuoni hapo.

Wanafunzi hao walikamatwa wakifanya maandamano kutoka chuoni hapo kuelekea katika ofisi mbalimbali za viongozi wa Serikali zilizopo Dodoma mjini majira ya saa kumi na moja alfajiri.
 
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, David Misime alisema wahusika wa vurugu hizo ni wanafunzi wa programu maalumu ya diploma ya ualimu.
 
Imeelezwa kuwa awali wanafunzi hao juzi walifanya kikao ambapo walitoka na maazimio ya kudai ongezeko la posho ya chakula na kupinga kucheleweshwa malipo hayo.
 
Pamoja na kutoka na madai hayo yaliyofikishwa kwa uongozi, uongozi uliwaeleza kuwa wenye mamlaka ya kuzungumzia suala la kuongezewa posho ni Bodi ya Mikopo na siyo chuo na kuwataka kufuata taratibu kuwasilisha madai yao.
 
Hata hivyo, walielezwa kuwa hundi kwa ajili ya fedha za posho zao zimeshasainiwa na kuwasilishwa benki ili waweze kuanza kupewa posho zao, lakini hawakuridhika.
 
“Hata hivyo, wanafunzi hao hawakuridhika na usiku wakaanza kuhamasishana kufanya maandamano jambo ambalo ni kosa kisheria,” alisema Kamanda Misime.
 
Aliongeza kuwa, wanafunzi hao wamehojiwa kulingana na ushahidi ambao umekusanywa na wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kufanya maandamano yasiyo na kibali.
 
Aidha, alisema viongozi waliohamasisha uvunjifu huo wa sheria baadhi yao wamekamatwa na baadhi wanaendelea kutafutwa ili nao waweze kuchukuliwa hatua stahiki.
 
Ushahidi uliokusanywa unaonesha jinsi viongozi hao wameshiriki kuhamasisha kupitia vikao rasmi na visivyo rasmi, katika vikundi, kupita katika mabweni na kutuma ujumbe mfupi wa simu (SMS).
 
Kamanda huyo wa Polisi alitoa wito kwa wanafunzi hao kutumia taratibu zilizowekwa na Serikali na Chuo kuwasilisha malalamiko yao ngazi kwa ngazi na siyo kufanya vitendo vya kuvunja sheria ambavyo vitawasababishia kupambana na vyombo vya dola.
 
Wanafunzi hao ambao ni wa programu maalumu kwa ajili ya walimu wa masomo ya Hesabu, Fizikia, Kemia, Baiolojia na Tehama yenye wanafunzi zaidi ya 3,000 wanasema wataendelea na maandamano na mgomo wakitaka kumuona Rais au Waziri Mkuu ambao ndio wamekuwa wakihimiza programu hiyo maalumu.
 
Mmoja wa wanafunzi hao, Yuda Mases akizungumza na gazeti hili alisema maandamano yao yaliyokuwa ya amani yalikumbana na vikwazo vya polisi ambavyo vilifanya waingie mjini kwa mtindo wa makundi.
 
Alisema wenzao wapatao 100 akiwemo Rais na Waziri Mkuu wa Serikali ya Udom programu maalumu wametiwa mbaroni katika juhudi za wazi za wanafunzi hao kutaka serikali iwaangalie kutokana na kukosa fedha za chakula ambazo zimechukuliwa na Chuo Kikuu cha UDOM.
 
“Tangu Novemba 8, mwaka jana tumefika hapa tumelipwa Sh 367,500 kama hela ya chakula kwa siku 60 kamili, lakini fedha hizo zilikatwa na UDOM Sh 282,500 kama Direct Cost na hii imeleta shida kwa wanafunzi,” alisema Moses ambaye amedai kuwa kwa sasa kila siku mbili watu wanaanguka kwa kukosa chakula.
 
Alisema maandamano yao ni kutaka kuwaambia viongozi waliosimamia programu hiyo maalumu Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda waone haki inatendeka kuhusu fedha, malazi, vitabu na vitamkwa (vilivyoorodheshwa katika barua za kuwaita).
 
Alisema kwamba programu hiyo ina watu takribani 3,000 wakiwa wametawanyika katika vitivo vitatu vya Tehama, Elimu na Sayansi Jamii.
 
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idrisa Kikula hakupatikana kuzungumzia suala hilo, kwani alipotafutwa ilielezwa yupo kwenye kikao.

Post a Comment

0 Comments