Business

header ads

MUUZA CHIPS APATA NISHANI YA RAIS

Rais Jakaya Kikwete jana aliwatunuku nishati Watanzania 28, akiwamo muuza chips, Kassim Said Kassim (28), ambaye aliyepewa nishani na ushupavu baada ya kupambana na kumdhibiti jambazi mwenye silaha.

Hafla ya utoaji wa nishani hizo ilifanyika jana jioni katika Viwanja vya Ikulu na kuhudhuriwa na mabalozi na viongozi mbalimbali wa Serikali, huku Kassim akiwa kivutio kutokana na idadi kubwa ya watu kushangazwa na ujasiri wake wa kupambana na jambazi mwenye silaha.

Kijana huyo alikuwa wa mwisho kutajwa na baada ya mshereheshaji wa hafla hiyo kueleza historia yake kwa kifupi kwamba alizaliwa mwaka 1986, iliibuka miguno kutoka kwa wageni waliohudhuria hafla hiyo na aliposimulia kisa chenyewe, kila mtu aliduwaa. Baadaye Kassim alimweleza mwandishi wetu: “Nilikuwa nafanya biashara ya chips eneo la Buguruni Malapa. Nakumbuka Julai 7, mwaka jana saa tatu usiku tulivamiwa na jambazi aliyekuwa na bastola na kuanza kuwatishia wateja, akitaka kupatiwa fedha na vitu mbalimbali.

“Kwanza alianza kuwashinikiza wateja wampatie fedha na alipoona hakuna aliyemsikiliza, alichomoa bastola na kumtishia mmoja wa wateja, hapo ndipo nilipoamua kupambana naye.”
Alisema alichukua chepe na kumpiga nalo mara mbili sehemu ya kichwani hadi alipoanguka na kuzirai. Alisema baada ya hapo, alitoa ripoti polisi ambao walifika na kumchukua.
Viongozi waliotunukiwa Nishani ya Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Muungano Daraja la Pili ni Adam Sapi 

Mkwawa (marehemu), Erasto Man’genya (marehemu), Pius Msekwa, Samuel Sitta, Francis Nyalali (marehemu), Augustino Ramadhani, Timoth Apiyo (marehemu), Paul Rupia, Ali Salum Ahmed na Mohammed Fakih Mohammed.

Waliopewa Nishani ya Kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano Daraja la Tatu ni Peter Kisumo, Anna Abdallah, Kingunge Ngombare-Mwiru, Isaack Sepetu (marehemu), Alli Mzee Alli (marehemu), Brigedia Jenerali mstaafu Adam Mwakanjuki (marehemu). Ali Ameir Mohamed, Al-Noor Kassum, Jenerali mstaafu Ernest Kiaro (marehemu), Solomon Liani (marehemu), Augustine Mahiga, Phillemon Mgaya, Ambindwile Mwaijande (marehemu) na Simeon Mwanguku.

Waliopewa Nishani ya Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Muungano Daraja la Nne ni Sophia Kawawa (marehemu), Haji Machano Haji, Johari Yusufu Akida na Bendi ya Atomic Jazz. Jenerali mstaafu David Musuguri alipewa Nishani ya Operesheni Safisha Msumbiji huku Kassim akipewa nishani ya ushupavu.
SOURCE: MWANANCHI

Post a Comment

0 Comments