Business

header ads

VIWANDA, KILIMO VYATAJWA KUKUZA PATO LA TAIFA KWA ASILIMIA 6.9


Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Morrice Oyuke (katikati) akizungumza  na waandishi wa habari kuhusu ukuaji wa Pato la Taifa kwa bei ya Soko leo jijini Dar es salaam. Wengine ni Bw. Fred Matola, Mtakwimu Mkuu Takwimu za Uchumi (kushoto), Bi. Adella Ndesangia (wa pili kutoka kulia) ambaye ni Mtwakimu Mkuu wa Ofisi hiyo na Bi. Jovitha Rugemalila.  Sekta za Kilimo,Viwanda, Biashara za jumla na rejareja zimetajwa kuongoza katika kuchangia kukua kwa pato la Taifa kwa asilimia 6.9 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2014.

Akitoa taarifa ya kukua kwa pato la Taifa leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Morrice Oyuke amesema kuwa kuanzia mwezi Aprili hadi Juni 2014 sekta hizo zimetoa mchango mkubwa wa kukuza pato la Taifa. 

Amesema ukusanyaji wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya uzalishaji uliofanywa na wataalam wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuzingatia  kanuni za kimataifa za kukokotoa pato la Taifa  unaonyesha kuwa jumla ya thamani ya pato hilo imefikia kiasi cha shilingi trilioni 5.4 ikilinganishwa na trilioni 5.0 za mwaka 2013.

Bw. Oyuke amesema  katika kipindi hicho shughuli za kilimo cha mazao zimekua na kufikia asilimia 6.5 ikilinganishwa na 5.4  za mwaka uliopita huku mifugo ikifikia asilimia 0.9,  misitu na uwindaji zikifikia asilimia 0.8,  shughuli za uvuvi zikikua kwa asilimia 2.1.
Ameongeza shughuli za uchimbaji wa madini ya Almasi, Tanzanite, mawe, na kokoto zimechangia kukua kwa pato la taifa  kwa kasi ya asilimia 3.0 katika kipindi hicho ikilinganishwa na asilimia 2.6 za kipindi kilichopita.

Aidha, amesema sekta ya uzalishaji wa bidhaa za viwandani imekua kwa asilimia 7.0 ikilinganishwa na 6.6 za mwaka uliopita kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji na uhifadhi wa bidhaa za nyama, samaki, matunda, mboga za majani na mafuta.
Shughuli nyingine zinahusisha uzalishaji wa bidhaa za vyakula, nguo na simenti, utoaji wa huduma na uchumi zikiwemo za ukarabati wa magari, pikipiki na vifaa vingine vya majumbani zikikua kwa asilimia 7.1 ikilinganishwa na asilimia 6.6 ya kipindi kama hicho kwa mwaka 2013.

Bw. Oyuke ameeleza kuwa shughuli za uchukuzi na mawasiliano zimekua na kufikia  asilimia 16.8 katika kipindi hicho huku huduma za hoteli na migahawa zikifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 4.0, shughuli za uendeshaji wa Serikali zikiwa asilimia 4.8, Elimu asilimia 6.3, huduma za afya na  shughuli nyingine zikikua kwa asilimia 4.8.

Amebainisha kuwa sekta ya umeme katika robo ya pili mwaka 2014 imeendelea kukua kutokana na kupatikana kwa vyanzo mbadala vya kuzalisha umeme hususan ugunduzi na matumizi ya gesi nchini ambayo yameondoa tatizo la utegemezi wa umeme wa maji katika kuzalisha umeme.

“Kwa kipindi kirefu sekta ya umeme imekuwa na mawimbi kwa kiasi kikubwa , umeme wetu umekuwa wa kutegemea maji ya mvua, baada ya juhudi za Serikali na kugundulika kwa nishati ya Gesi nchini na kupatikana chanzo mbadala cha nishati tatizo hili limeshghulikiwa sasa sekta hii imeimarika” Amesema.

Amesema Tanzania sasa inafanya vizuri kiuchumi katika nchi za Afrika ya Mashariki kwa kuendelea kushika nafasi ya pili ikifuatiwa na Uganda, Rwanda na Burundi na kuongeza kuwa hali ya amani na utulivu iliyopo nchini inaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kukua zaidi kiuchumi.

Aidha  amefafanua kuwa katika Afrika Mashariki, Tanzania inaendelea kufanya vizuri  katika sekta ya utalii kwa kuwa na ongezeko la idadi ya watalii wanaoingia nchini kutokana na hali ya usalama na amani  iliyopo .

Post a Comment

0 Comments