Business

header ads

TUWAPENDE WATOTO WENYE UTINDIO WA UBONGO


Kama alivyo mlemavu mwingine, mtoto mwenye tatizo la mtindio wa ubongo anahitaji kupendwa, kuthaminiwa na kusaidiwa na jamii inayomzunguka, ajisikie mwenye furaha na amani kama binadamu mwingine yeyote asiye na tatizo katika maumbile yake.


Katika kuadhimisha siku hii Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya afya imevikutanisha vikundi mbalimbali katika kujadili badhi ya changamoto zinazowakumba wale wenye matatizo haya na wakiwemo walezi wao. Nikiwa katika pilikapilika za kutafuta habari nimefika katika uwanja wa Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam na kuwakuta wakina mama wakiwa na watoto wao na kueleza baadhi ya changamoto wanazokutana nazo katika kuhakikisha watoto hao wanapata malezi bora.

Mmoja wa wanakikundi cha wazazi wenye watoto wenye utindio wa ubongo aishie Tegeta ameeleza jinsio wanavyoteseka kutokana na jamii kuwatenga na kufanya watoto hao kukosa huduma muhimu ikiwemo za elimu mama huyo ameeleza changamoto kubwa wanayopata ni ya usafiri na kueleza wanakosa msaada kutokana na mzazi mwenzi kukimbia na kueleza kuwa hawakuwahi kuwa na mtoto wa aina hiyo katika ukoo wao.

Mwandishi Nansembaeli Mduma anaeleza zaidi
Inaelezwa kuwa kuna baadhi ya wanajamii wanawatazama wazazi wa watoto wenye ulemavu huo kwa jicho tofauti, lenye maswali mengi kuhusu sababu za kuwazaa.

Tena inazungumzwa kuwa wapo wanaoamini kwamba kwa namna yoyote ile, hawawezi kuzaa watoto wa aina hiyo, ndio maana kutwa kucha, wanawanyooshea vidole wakifikiri kuwa huenda wameumbwa kwa mazingira ya kishirikina au kutokana na laana.
Huo ni mtazamo hasi usiompendeza Mungu wala binadamu mwingine, mwenye moyo wa huruma na uelewa uliokomaa kwamba si rahisi mama au baba akapanga kuwa na mtoto mwenye mtindio wa ubongo.

Nilisikiliza mazungumzo ya mama wa mtoto wa kike wa miaka 10, aliye na mtindio wa ubongo wakati akihojiwa na kipindi cha televisheni moja ya nchini, nikaona haja ya kuwashirikisha Watanzania kufahamu mambo machache kuhusu umuhimu wa kuwasaidia watoto hao.

Ni Mwanahamisi Hussein anayehudumia katika kituo cha kulea watoto wenye ulemavu huo katika eneo la Manzese, Dar es Salaam.
Alieleza kuwa uzoefu alioupata kwa mwanawe, umemdhihirishia kuwa upendo wa dhati wa wazazi, ndugu, jamaa, marafiki na wana jamii wengine, unaweza kumfanya mtoto mgonjwa pamoja na wanaomhudumia, kupunguza machungu wanayoyapata kwa kushuhudia namna uendeshaji wa maisha kwa watoto wenyewe unavyokuwa mgumu, pindi wanapokosa mtu karibu yao.
Hussein anasema baadhi ya wazazi wanakatishwa tamaa na wanajamii wanaowazunguka, pindi wanapoonesha dhamira ya kuwatafutia matibabu na elimu.
Anasema, wapo wanaowaambia wazi kuwa watoto hao hawatawasaidia kwa lolote maishani, kutokana na ulemavu wao, kwa hiyo hawana haja ya kuhangaika au kuingia gharama kuwatafutia elimu.

Binafsi ninawachukulia wanaotoa ushauri huo mbaya kuwa ni wajinga, wenye kuhitaji kuelimisha wafahamu kwa nini walemavu wa ubongo, nao wanapaswa kuchanganywa na wenzao.

Ikumbukwe kuwa mtoto mwenye tatizo hilo la kimaumbile, akitengwa kwa kufungiwa ndani au kutoruhusiwa kujichanganya na wenzake, anakuwa na uwezekano mkubwa wa kuendelea kuumizwa na tatizo, tofauti na jinsi baadhi ya watu wanavyofikiri.

Anapofikishwa kwenye vituo vya mazoezi, anakuwa ametoka katika aina moja ya mazingira na kuingia kwenye nyingine.
Pia, anakuwa anakutana na watu tofauti, hata kama hataweza kuwakumbuka au kuchukua mawasiliano yao kwa matumizi ya baadae ukubwani. Lakini, ieleweke pia kuwa si kila mtoto mwenye utindio wa ubongo, hatambui jema analotendewa.
Anaweza akashindwa kutafsiri maneno mabaya anayozungumziwa, lakini la faraja akalielewa na kulishika, hivyo iachwe tabia ya kuwanong’ona kwa kitazamo hasi na utengenezwe utamaduni mpya wa kuwasifu, kuwaonyesha kuwa bila wao mambo hayaendi na maneno mengine ya faraja.

Nampongeza sana mama huyo (Hussein) kwa ujasiri wake, kutokana na maneno aliyoyatamka kwenye mahojiano yale kwamba haelewi itakuwaje siku mwanawe akiondoka duniani.

Alisema wakati wote huwa naye na amemzoea, kiasi kwamba akikaa mbali naye kwa muda mrefu hujihisi kupungukiwa. Wakati anasema hivyo, nafahamu lazima watakuwepo wenye watoto kama huyo, wanaofikiria ni lini watapata mwanya ili wamtupe au wamtelekeze nap engine kumuua kabisa.

Hiyo ni roho ya shetani inayopaswa kupigwa marufuku haraka iwezekanavyo kwa sababu, kila binadamu, awe na viungo kamili au mwenye ulemavu, ana haki ya kuishi kutokana na jinsi Mungu anavyotaka.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema kila mtu ana haki ya kuishi, hivyo isifanyike kinyume cha hapo, kwa kuwa itakuwa ni kumchukiza Mungu na kuvunja sheria za nchi.
Tumekuwa tukiimbiwa nyimbo zenye mafunzo kuwa mtoto ni mtoto hata awe mlemavu, sasa iweje wengine wafananishwe na mizigo? Ni kosa na ukosefu wa adabu, kumfananisha binadamu na kitu kisicho na uhai.
Nasisitiza jamii iwapende na kuwathamini wenye utindio wa ubongo, kwa sababu wana haki ya kupendwa na kuthaminiwa kama wengine.

Post a Comment

0 Comments