Business

header ads

NDOA ZA UTOTONI KUONGEZEKA

Katibu Mtendaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Bi. Anna Tayari Maembe
Serikali ya Tanzania imesema ushiriki hafifu wa Wananchi katika kutoa taarifa za watoto wanaolewa nchini umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ndoa za utotoni hali inayopelekea watoto hao kukosa fursa ya kupata elimu.

Akiongea leo Jijini Dar es Salaam Katibu Mtendaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Bi. Anna Tayari Maembe wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha jamii kutokomeza ndoa za utotoni amesema baadhi ya jamii zilizopo katika kanda ya ziwa zimekuwa zikishiriki kuoza watoto wao na hivyo kuwahatarishia maisha yao huku sheria ya ndoa nayo ikiwa ni kikwazo.

"Mchakato wa katiba ukiisha naimani sheria iliyopo itafanyiwa marekebisho ili kuweza kuwadhibiti na kuweza kuwajibika kutokana na matendo yetu, natoa rai kwa wazazi kuanza kufanya mabadiliko kuanzia ngazi ya familia na kuepuka kufungisha ndoa watoto wadogo" alisema

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha waandishi wa Habari Wanawake nchini TAMWA, Bi. Valerie Msoka amesema usiri mkubwa uliopo miongoni mwa wazazi na walezi unaochangiwa na umasikini katika familia hizo umesababisha watoto wengi kuolewa wakiwa na umri usioweza kuongoza familia ambapo mkakati wa pamoja utasaidia kuondokana na hali hiyo 

"Bila kuwa na mpango maalumu au mkakati maalum hatutaweza kupambana na ndoa za utotoni kwa hiyo mkakati uliopo ni kutoa elimu kwa wazazi na watoto ili kuleta chachu ya mabadiliko na kuzifahamu changamoto zilizopo katika kutokomeza tatizo hilo"

Post a Comment

0 Comments