Business

header ads

WAKUU WA MIKOA NA MAKATIBU TAWALA WATAKIWA KUONDOA TOFAUTI ZAO


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiyafunguwa Mafunzo ya siku Tatu ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania bara  Jijini  Dar es Salaam.

Baadhi ya Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara wanaohudhuria mafunzo ya Uongozi wakifuatuilia Hotuba ya Mgeni rasmi wa ufunguzi wa mafunzo hayo Balozi Seif hayupo pichani.

Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara wanaohudhuria mafunzo ya siku tatu ya Uongozi yanayofanyika Hoteli ya White Sand Mjini Dar es Salaam.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiagwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh. Sadiq Meki Sadiq mara baada ya kuyafungua mafunzo ya siku tatu ya uongozi kwa wakuu wa mikoa ya Tanzania bara. Picha zote na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ


PRESS RELEASE:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa mawasiliano ya muingiliano wa kiutendaji kati ya Wakuu wa Mikoa na Maafisa Tawala wa Mikoa ndio masuala ya msingi yanayolalamikiwa na Wananchi ambayo husababisha huduma finyu zisizokidhi vinavyotolewa katika sekta za Umma.


Alisema hali hiyo husababisha ongezeko la rushwa, ubabaishaji wa baadhi ya watumishi katika kutoa maamuzi ya haraka ndio mambo yanayosababisha urasimu na ucheleweshaji wa mambo mbali mbali ya maendeleo ndani ya Mikoa.


Balozi Seif alisema hayo wakati akiyafunguwa mafunzo ya siku tatu ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara yanayofanyika katika Hoteli ya White Sand nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam.

Alisema zipo changamoto za mahusiano na muingiliano wa kiutendaji miongoni mwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ambazo husababisha baadhi ya Viongozi hao kutoa maamuzi peke yao na hatimae kuleta dosari katika utendaji wao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Mahusiano na Muingiliano wa utendaji kazi baina ya Viongozi wa Kisiasa na watendaji ni muhimu na yanahitajika kwa ajili ya kuimarisha Utawala bora pamoja na ukuaji wa Maendeleo ya Taifa.

“ Uhusiano nwa Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa hauishii kwenye utendaji kazi za kila siku bali hata kwenye upangaji wa Mipango ya na upimaji wa utendaji kazi wa nusu mwaka na ule wa mwaka mzima “. Alisema Balozi Seif.

Balozi Seif alisisitiza kwamba pande hizo mbili wakati wote zinategemeana katika utekelezajiwa ufanisi wa majukumu katika ngazi za Mkoa jambo linalohitajika kwa kila mmoja kuwa na imani kwa mwenzake kwa ajili ya kuendeleza uhusiano katika uwajibikaji.

Alieleza kwamba kinyume cha mategemeano hayo Mkoa unaohusika na mikwaruzano ya uwajibikaji utakosa muelekeo na hatma yake kusababisha msuguano.

Aliwanasihi Wakuu na Makatibu hao Tawala wa Mikoa kuitumia vyema fursa waliyoipata ili kubadilishana uzoefu na kujenga mtandao wa mawasiliano na mahusiano kwa ajili ya kupashana habari na kushauriana.

Aliwataka washiri hao wa mafunzo ya Mawasiliano ya muingiliano kujenga mshikamano wa maelewano utakaorahisisha utendaji na kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishauri Taasisi ya Uongozi kuona namna ya kuwahusisha Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya pamoja na viongozi wa Serikali za Mitaa katika mafunzo kama hayo ili kuwajengea uwezo wa uwajibikaji.

Balozi SDeif alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kutoa ushirikiano ili kuona mpango huo unafanikiwa na kuiwajengea nguvu za utoaji huduma kwa wananchi watendaji hao wa Serikali.

Alizishauri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa { TAMISEMI } pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum ya SMZ kushirikiana katika kulitekeleza suala hilo.

“ Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum TAMIM zione namna ya kuwajumuisha watendaji hao katika kuhudhuria mafunzo yenye kuboredha uongozi katika maeneo yao “. Alisema Balozi Seif.

Mapema Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Tanzania Profesa Joseph Semboja alisema mafunzo hayo ya siku tatu kwa Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara yataendeshwa kwa njia ya majadiliano.

Profesa Semboja Washiriki hao watapa fursa ya kubadilisha uzoefu pamoja na kutafuta mbinu za kuzitatua changamoto zinazoikabili Mikoa mbali mbali Nchini Tanzania.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kuyafungua mafunzo hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa { TAMISEMI } Mh. Hawa Ghasia alisema jumla ya Wakuu wa Mikoa 20 na Makatibu Tawala wa Mikoa 22 wanahudhuria mafunzo hayo.

Mh. Ghasia alisema Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa watakaokosa mafunzo hayo wanatarajiwa kuungana na Wakuu wa Mikoa na Maafisa Tawala wa Mikoa ya Zanzibar katika mafunzo yatakayotolewa hapo baadaye Zanzibar.Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

21/7/2014.


Post a Comment

0 Comments