Business

header ads

Albino auawa, wauaji watoweka na viungo

Watu wasiojulikana mkoani Simiyu wamemuua kwa kumkatakata mapanga mlemavu wa ngozi (albino), Mughu Lugata (40) huku wakitoweka na baadhi ya viungo vyake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 12:00 usiku nyumbani kwa Lugata katika Kitongoji cha Chalala, Kijiji cha Gasuma, Kata ya Nkololo wilayani Bariadi, mkoani hapa.


“Wauaji hao baada ya kumuua Lugata walimkata mguu wa kushoto na kuchukulia sehemu ya goti, vidole viwili vya mkono wa kushoto na kucha ya kidole gumba cha mkono wa kushoto na kuondoka navyo,” alisema Mkumbo.

Mkumbo alisema Lugata akiwa amelala peke yake nyumbani kwake, alivamiwa na watu wasiojulikana na kuanza kumkatakata mapanga na kuchukua baadhi ya viungo vyake vya mwili na kutokomea navyo kusikojulikana. Alisema tayari wanawashikilia watu wawili, mmoja akidaiwa kuwa ni mganga wa kinyeji mkulima wa kijiji hicho.

Mkumbo alisema mtuhumiwa mwingine alikuwa kwa mganga huyo wakiwa na vifaa vya kupigia ramli na kwamba chanzo cha tukio hilo ni imani za ushirikina.
Aliwataka wananchi wenye taarifa ya wahusika wa tukio hilo kuisaidia polisi ikiwamo kuacha kudanganyika kuwa utajiri unakuja kwa imani za ushirikina bali kufanya kazi kwa bidii.

Alisema kuna baadhi ya waganga wanawadanganya wateja wao kuwa, viungo vya walemavu wa ngozi vinaleta utajiri hali ambayo inawasababisha kuamini na kuendeleza mauaji hayo kwa albino.
Kasi ya mauaji dhidi ya albino lilikuwa limepungua baada ya Serikali na mashirika ya ndani na nje kupiga vita mauaji hayo, lakini tukio hili linaanza kutonesha vidonda na kuhatarisha usalama wa walemavu hao.
 SOURCE: MWANANCHI

Post a Comment

0 Comments