Business

header ads

MAANDALIZI YA MAONYESHO YA ASALI YAMEKAMILIKA


Maandalizi ya MAONYESHO YA ASALI YA DAR ES SALAAM (DAR ES SALAAM HONEY  EXHIBITION) ambayo yatafanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere (Sabasaba) Dar es Salaam tangu tarehe  3 hadi 7 Oktoba 2012 yamekamilika. Wananchi wanakaribishwa kuhudhuria maonyesho hayo ambayo hayatakuwa na kiingilio. Katika maonyesho hayo watu wataelimika kuhusu manufaa yatokanayo na asali, pia watapata utaalam wa kufuga nyuki na wataonja na kununua asali bora kwa bei nafuu.
Kaulimbiu ya maonyesho hayo ambayo ni ya kitaifa ni ASALI KWA AFYA NA USTAWI (HONEY FOR HEALTH AND PROSPERITY). Maonyesho hayo yameandaliwa  kwa ushirikiano wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade)  na wadau wengine wa Sekta ya Ufugaji Nyuki. Lengo kuu la maonesho ni kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya nyuki.
Tarehe 3 Oktoba ni siku iliyotengwa maalum kwa ajili ya kufanyika Kongamano la Ufugaji Nyuki. Hivyo wafugaji nyuki, wataalam na wadau mbalimbali wa Sekta hiyo wanakaribishwa kuhudhuria kungamano hilo ambalo litafanyika katika ukumbi wa J. M. Kikwete ulioko kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere .
Ufunguzi rasmi wa maonyesho hayo utafanyika tarehe 5 Oktoba 2012  ambapo Mgeni Rasmi anategemewa kuwa Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Peter Pinda (Mb).
Waonyeshaji waliothibitisha kushiriki ni Halmashauri za Wilaya zote, kampuni zinazonunua asali, watengenezaji wa mizinga na vifaa vingine vya kisasa  vya ufugaji nyuki, na watengenezaji wa bidhaa zinaotumia asali na nta kama malighafi.
Inategemewa kuwa katika maonyesho hayo waonyeshaji watajitangaza ili waweze kupata wanunuzi wa asali na mazao mengine ya nyuki. Pia wanunuzi wa mazao ya nyuki watapata fursa ya kuwafahamu wafugaji. Aidha inategemewa kuwa utaundwa mtandao ambao utawaunganisha wazalishaji, wafanyabiashara, wataalam na wadau wa sekta ya nyuki.

George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
30 Septemba 2012
                                                   Simu: +255 784 468047

Post a Comment

0 Comments