Business

header ads

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI TOKA TFF

TAREHE 25/09/2012
 
Tumepokea barua kutoka Kitengo cha Sheria cha Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpirawa Miguu (FIFA) likitutaka tuitaarifu Yanga kuhusu mashtaka yaliyowasilishwa na kocha wazamani wa klabu ya Yanga, Kostadin Papic. Katika malalamiko yake, Papic anadai kuwa hajalipwa malimbikizo ya mshahara wake yanayofikia kiasi cha Dola 12,300 za Kimarekani. Katika barua yake, kocha huyo anadai kuwa alikuwa akiwasiliana na maofisa na viongozi waYanga, lakini hakupata ushirikiano na hivyo kuamua kwenda FIFA. TFF ilifanya juhudi za kuwasiliana na Yanga kuhusu malalamiko hayo ili kujaribu kumzuia kocha huyo asishtaki FIFA, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.
 
Kama chombo kinachosimamia uendeshaji wa mpira wa miguu nchini, TFF imesikitishwa na habari hizo na inaiomba klabu ya Yanga kufanya kila jitihada kuhakikisha kuwa inawasilishataarifa zote muhimu na nyaraka zinazohusiana na stahiki za kocha huyo ili kama ilishamalizana naye, sifa ya klabu ya Yanga isafishwe. Tayari barua imeshaandikwa kwa klabu ya Yanga kuitaka itekeleze utashi huo mapemz iwezekanavyo.
 
Tukio hilo, si tu linachafua sifa ya klabu ya Yanga, bali soka ya Tanzania kwa ujumla kutokana na ukweli kwamba ikishadhihirika kuwa kuna tatizo la malipo ya makocha nchini, ni dhahiri kuwa itakuwa ni vigumu kwa klabu zetu na hata timu za taifa kupata makocha wazuri kutoka nje kwa kuwa watakuwa wamejengeka hofu ya kufanya kazi nchini.
 
Hili ni tukio la pili kwa Yanga baada ya mchezaji wake mwingine, John Njoroge kuishtaki klabu hiyo FIFA na kushinda kesi yake iliyoamuliwa mwezi Januari na Kitengo cha Usuluhishi wa Migogoro cha FIFA (DRC). Ushindi wa Njoroge unamaanisha kuwa iwapo Yanga itashindwa kutekeleza kumlipa mchezaji huyo kasi cha Sh milioni 17, inaweza kujikuta katika adhabu ambayo itatulazimisha tuishushe daraja; kuinyang’anya pointi kwa kiwango kitakachotajwa na FIFA; kuipiga faini au adhabu zote kwenda kwa pamoja. Tunaiomba Yanga itekeleze hukumu hiyo kwa wakati uliotajwa kwenye barua ya FIFA ili kuepuka hatua hizo.
 
Suala la Njoroge ni moja kati ya matukio mengi yanayohusu ukiukwaji wa taratibu za kuvunja mikataba yanayofanywa na klabu zetu. Kuna malalamiko ya wachezaji wengi dhidi ya klabu zao za zamani kuhusu kutolipwa stahiki zao. Hivyo TFF inatoa wito kwa klabu kujiepusha na vitendo hivyo kwa kuwa vinawanyima haki wachezaji, lakini pia vinachafua sifa ya nchi iwapo wachezaji wanachukua hatua za kwenda kwenye vyombo vya juu.
 
Tumekuwa tukisoma kwenye vyombo vya habari kuhusu kutimuliwa kwa sekretarieti nzima ya Yanga kutokana na kuonekana kuwa ina udhaifu. Taarifa hizo hazijaifikia rasmi TFF. Kiutaratibu, Yanga inatakiwa iwsasilishe majina ya maofisa watakaofanya kazi na TFF kwa sasa na itakapoajiri sekretarieti ya kudumu, basi itume barua nyingine ya kuwatambulisha watendaji wake.
 
 
 
 
Kama itakuwa imeitimua sekretarieti nzima, basi TFF inapokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa. Si nia ya TFF kutetea watendaji wazembe, lakini klabu hazina budi kufuatilia kwa karibu utendaji wa sekretarieti zao ili isije ikafikia wakati sekretarieti nzima inaondolewa kwa makosa ambayo yangeweza kusahihishwa kama kungekuwa na ufuatiliaji wa karibu. TFF imekuwa ikitoa mafunzo kwa watendaji wa klabu ili waweze kufanya kazi zao vizuri na kwa mintaarafu ya mpira wa miguu na hivyo kuondolewa kwa timu nzima kama hiyo kunamaanisha kuwa ni upotevu wa rasilimali ambayo imetumika kuwapa elimu ya kutenda kazi zao vizuri. TFF ilishafanya kozi ya Event Management kwa ajili ya watendaji wa klabu; semina ya kuangalia upya maazimio ya Bagamoyo kwa watendaji na viongozi na pia kozi ya utawala hivyo haipendi juhudi hizi zipotee kirahisi.
 
 
Angetile Osiah
KATIBU MKUU
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Septemba 25, 2012
 
LIGI KUU VODACOM KUENDELEA KESHO
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Septemba 26 mwaka huu) kwa mechi mbili zitakazochezwa katika miji ya Tanga na Morogoro.
 
Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Polisi Morogoro na Toto Africans ya Mwanza. Polisi Morogoro ambayo imepanda daraja msimu huu imeshacheza mechi tatu na kufanikiwa kupata pointi moja tu baada ya kutoka suluhu na Mtibwa Sugar katika mechi ya kwanza.
 
Nayo Toto Africans ambayo katika mechi iliyopita ugenini ililazimisha suluhu dhidi ya Coastal Union, yenyewe ina pointi tatu baada ya kutoka sare katika mechi zote tatu ilizocheza chini ya kocha John Tegete.
 
Mechi nyingine ya ligi hiyo itakuwa kati ya Coastal Union ambayo itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Kagera Sugar inayofundishwa na Abdallah Kibaden, wikiendi iliyopita iliondoka na pointi zote tatu kwenye uwanja huo baada ya kuifunga Mgambo Shooting bao 1-0.
 
Ligi hiyo itaingia kwenye Super Weekend kuanzia Ijumaa (Septemba 28 mwaka huu) kwa mechi kati ya Azam na JKT Ruvu itakayochezwa Uwanja wa Taifa itaoneshwa moja kwa moja (live) na kituo cha SuperSport kuanzia saa 1 kamili usiku.
 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Post a Comment

0 Comments