Business

header ads

JAJI MKUU AWAAPISHA JUMLA YA MAHAKIMU WAPYA 372

 Jaji Mkuu wa Tanzania, akiwapa nasaha Mahakimu wapya mara baada ya kuwaapisha Mahakimu hao (angalia chini ) hivi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) kilichopo Lushoto-Tanga.
Picha na mdau Mary Gwera wa  Mahakama)

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman amewaapisha na kuwaasa juu ya utendaji kazi Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo walioajiriwa hivi karibuni.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Mahakimu 372  katika hafla iliyofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) wilayani Lushoto hivi karibu, Mhe. Chande alisema kuwa Mahakimu hao watumie fursa waliyoipata katika kutoa haki sawa na kwa wakati stahiki.
“Mahakama imejiwekea mkakati wa kuajiri Mahakimu wenye shahada ya Sheria, na kwa mara ya kwanza tumefanikiwa kuajiri jumla ya Mahakimu 300 wenye shahada ya sheria, hivyo, Mahakama na jamii kwa ujumla ina matumaini makubwa juu ya ujio wenu katika suala zima la utoaji haki,” alibainisha Jaji Mkuu.
Alisema kuwa asilimia 70 ya mashauri yapo katika Mahakama za Mwanzo jambo ambalo linapelekea wingi la mashauri na hivyo kuwataka Mahakimu kusikiliza na kuzitolea maamuzi kwa wakati kesi ambazo ushahidi tayari wake umekamilika.
Aliongeza kwa kutaja sifa za Hakimu bora na kuainisha kuwa anatakiwa kuwa anayetoa maamuzi kwa kuzingatia haki, sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
“Hakimu bora anatakiwa pia kulinda heshima ya Mahakama na taaluma  yake na ya Mahakimu wenzake, pamoja na kuheshimu wajibu wake kwenye jamii husika na vilevile kufuata maadili ya kazi katika suala la utoaji haki,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Jaji Kiongozi, Mhe. Fakih Jundu aliwaasa pia Mahakimu hao kuzingatia haki za washitakiwa ikiwemo upatikanaji wa dhamana endapo mshitakiwa husika anastahili.
“Ni muhimu kwenu kuzingatia haki za washitakiwa na kuepuka matumizi mabaya ya vifungu vya sheria, mkifanya hivyo mtajiweka katika nafasi  nzuri ya kufanya maamuzi ambayo hayakiuki misingi ya haki,” alisema Jaji Kiongozi.
Sambasamba ya shughuli ya kuwaapisha Mahakimu hao, pia wamepata mafunzo ya wiki moja kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Mahakama juu ya utendaji kazi wa kila siku hususani suala zima la utoaji haki nchini.
Jumla ya Mahakimu 372 wameapishwa na Mhe. Jaji Mkuu, kuwa Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo zilizoko katika vituo mbalimbali nchini, Mahakimu 72 ambao walikuwa tayari kazini wameapishwa pia kuwa Mahakimu Wakazi baada ya kupata Shahada ya Sheria.
<

Post a Comment

0 Comments