KAMPUNI ya mawasiliano nchini ya
Airtel imeahidi kuendelea
kusaidia michezo mbalimbali nchini ikiwa na lengo la kukuza maendeleo ya
vijana.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika hafla fupi ya
kukabidhi shilingi milioni tano pamoja na fulana mia moja kama udhamini
wa mbio za Rock City Marathon za mwaka huu zenge kauli mbiu ‘tukuze
utalii wa ndani kupitia michezo’, Afisa Uhusiano wa Airtel, Bi Jane
Matinde alisema kuwa kampuni yake itaendelea kusaidia michezo mbalimbali
nchini ikiwemo riadha ili kukuza maendeleo ya vijana.
“Udhamini wetu wa shilingi milioni tano pamoja fulana mia moja
katika mbio za Rock City mwaka huu unalenga katika kusukuma maendeleo ya
vijana kupitia michezo kwa tunaamini kuwa michezo imekuwa ni chanzo
kikubwa cha ajira duniani.
“Tunaahidi kuendelea kusaidia michezo mingine kwa kuwa pia
tunaamini kupitia michezo mbalimbali tunaweza kutangaza vivutio vyetu
vya utalii duniani. Mfano nzuri ni mbio za mwaka huu za Rock City
Marathon zitakazowakutanisha wanariadha mbalimbali kutoka nchi jirani,”
aliongeza Bi. Matinde.
Akipokea hundi na fulana hizo, Mratibu wa mbio hizo kutoka
katika kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bi. Grace Sanga
aliishukuru kampuni ya Airtel kwa kuendelea kusaidia mbio za Rock City
na kuyahasa mashirikia na makampuni mengine kuiga mfano wa kampuni hiyo.
“Tunaishukuru Airtel kwa msaada wao kwa kuwa msaada huu
utatusaidia tujiandae vizuri na Rock City Marathon ya mwaka huu
itakayofanyika Oktoba tarehe 28 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini
Mwanza,” alisema Grace.
Grace alisema kuwa mbali na Airtel wadhamini wengine ni pamoja
na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Parastal Pension Fund (PPF),
Geita Gold Mine, African Barrick Gold, Air Tanzania Company Ltd (ATCL),
Mamlaka ya Taifa ya Mbuga za Wanyama nchini (TANAPA), Bodi ya Utalii
Tanzania (TTB), Nyanza Bottles, New Africa Hotel na New Mwanza Hotel.
Aidha, Bi Sanga aliwaasa wanariadha kujitokeza na kuanza
kujisajili ili kushiriki katika mbio hizo na kusema kuwa fomu za usajili
zinapatikana katika ofisi za uwanja wa CCM Kirumba, ofisi za kampuni ya
Capital Plus International zilizopo katika jengo la ATCL ghorofa ya
tatu, ofisi za Bodi ya Utalii jengo la IPS ghorofa ya tatu, Dar es
Salaam, na zinapatikana katika tovuti ya www.rockcitymarathon.blogspot.com.
CPI ilitangaza kuwa atakaeibuka kinara katika mbio za kilometa
21 mwaka huu kwa wanaume na wanawake atazawadiwa shilingi milioni moja
na laki mbili wakati mshindi wa pili ataweka mfuko shilingi laki tisa na
mshindi wa tatu ataondoka na shilingi laki saba.
0 Comments