Business

header ads

PROFESA MAHALU ASHINDA KESI YA UHUJUMU UCHUMI

Wanahabari wakitaka kupata maelezo toka kwa Profesa Mahalu (katikati) baada ya kushinda kesi yake leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, ameshinda kesi iliyokuwa inamkabili  baada ya kuonekana ushahidi uliotolewa na upande wa walalamikaji kutojitosheleza.
Akisoma hukumu hiyo leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hakimu Ilvine Mugeta, alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili amebaini kuwa Profesa Mahalu  na  aliyekuwa Mkuu wa Fedha na Utawala katika ubalozi huo, Grace Martin, hawana hatia na hivyo kuwaachia huru.
Hakimu Mugeta alisema kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa walalamikaji unajichanganya na kuonekana wazi kuwa tuhuma zilizokuwa zinamkabili Profesa Mahalu si za kweli.
Prof. Mahalu aliyekuwa anatetewa na wakili mkongwe Mabere Marando na wenzake alikuwa akikabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60, katika mchakato wa ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.
Awali, hukumu hiyo ilipangwa kusomwa Julai 11, mwaka huu lakini iliahirishwa kutokana na Hakimu Mugeta kukabiliwa na majukumu mengine. Kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana na kuipangia hukumu hiyo leo.
Akizungumza na  paparazi mara baada ya kushinda kesi hiyo, Profesa Mahalu alisema siri ya ushindi huo ni maombi aliyoyafanya kwa muda mrefu huku akisimamia kitabu cha Zaburi 17 ambacho ndiyo anaamini kimemsaidi kuibuka mshindi leo.
Wakati wa utetezi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye ununuzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wa uongozi wake, alipanda kizimbani na kumtetea Profesa Mahalu na mwenzake, akidai kuwa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo ulifuata sheria.
Akiongozwa na mmoja wa mawakili wanaomtetea Profesa Mahalu na mwenzake, Alex Mgongolwa, Mkapa alieleza mchakato wote wa ununuzi wa jengo hilo na malipo yake kwa kuwa lilinunuliwa kwa maagizo ya serikali yake.
Martin katika utetezi wake alidai kuwa, Profesa Mahalu hakuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 milioni, bali alililetea taifa faida kwa kuwa na jengo zuri na kwamba anahitaji kupewa shukrani.
Akiongozwa na Wakili Marando dhidi ya tuhuma zinazomkabili, Grace alidai: “Mheshimiwa kwa ufahamu wangu, Balozi Mahalu mashtaka yote sita yanayomkabili hakuyatenda, kwani aliwasilisha mikataba miwili kama taarifa iliyofanyika kihalali.”
Na George Kayala

Post a Comment

0 Comments