Business

header ads

WANASAYANSI WASEMA SILAHA ZOTE ZA KUKABILI VVU WANAZO


WASEMA SILAHA ZOTE ZA KUKABILI VVU WANAZO, WAOMBA FEDHA WAINGIE
WANASAYANSI mbalimbali wanaoendesha tafiti mbalimbali za kutafuta tiba na chanjo ya Ukimwi, wameitangazia dunia kuwa hatua waliyofikia sasa wanauona ugonjwa huo ‘siyo hatari tena’ kwa sababu wanazo silaha zote za kuweza kukabiliana nao.
Ila wakasema, kinachowakwamisha ni ukosefu wa fedha ambazo zinahitajika katika kuendeleza tafiti na kuweka sera mpya za kukabili Virusi Vya Ukimwi (VVU) duniani.
Hayo yalibainika kwenye siku ya pili ya Mkutano wa 19 wa Kimataifa wa Ukimwi unaofanyika mjini Washington DC, Marekani na unahudhuriwa na watu zaidi 22,000 miongoni mwao wakiwamo wataalamu wa afya, watunga sera na wadau wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo toka karibu kila kona ya dunia.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari cha Mkutano huo na gazeti hili kufanikiwa kupata nakala yake, ilieleza kwamba jopo la wanasayansi nguli duniani walikiri kuwa wamefanyia VVU utafiti wa kutosha ndiyo maana wanatamba kuwa wamefanikiwa katika kuvidhibiti.
“Kwa sasa tunazo silaha zote za kisayansi kumalizia mbali gonjwa hili la Ukimwi. Kilichobaki ni kutumia kikamilifu utaalamu huu katika fursa hii tuliyo nayo,” alisema Rais wa Taasisi ya Kijamii ya Kimataifa ya Mapambano dhidi ya VVU (IAS), Dk Elly Katabira.
Kiongozi huyo ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Mkutano huo akitokea nchini Uganda, aliongeza: “Kufanikisha hilo ni lazima tukubali kubadili mfumo kwa maana kwamba kuweka sera mpya zitakazowezesha kuokoa kundi linaloathirika zaidi na ugonjwa huu.”
Dk Katabira alifafanua: “Kinachohitajika ni kuweka mfumo utakaowashirikisha wafadhili na watunga sera katika kuweka mpango mzuri wa pamoja tuweza kulimaliza tatizo kwa silaha hizi za kisayansi.”
Naye Mtaalamu wa Tiba katika Chuo Kikuu cha California, Profesa Diane Havlir alisema: “Ujumbe wangu kwenu, hasa kwa watunga sera ni kwamba: endeleeni kuwekeza katika mipango ya kisayansi.”
Kwenye mkutano huo walishiriki pia wanasayansi wenye dawa na ushahidi unaoonyesha kuwa katika miaka ya karibuni zimeonyesha dalili nzuri za kutibu Ukimwi na kifua kikuu (TB).
Wataalamu wengi wa afya waliunga mkono kauli hiyo wakisema kwa sasa kuna uelewa mkubwa wa kitaalamu juu ya muundo na tabia ya VVU hivyo ni rahisi kwao kutengeneza dawa kwa ajili ya kuzuia, kutibu na chanjo.
Tafiti za awali
Kauli ya wanasayansi hao imekuja baada ya miaka 30 ya kipindi kigumu cha kutafiti namna ya kupata chanjo au tiba ya ugonjwa huo ambao umeua mamilioni ya watu duniani, hususan wataalamu na nguvu kazi inayohitajika kuimarisha uchumi.
Waligundua VVU mwaka 1981 na ilikuwa vigumu kupata dawa ya kuviua kwa sababu ya tabia zao na uwezo wa kujigeuza kuwa sehemu ya mwili na kutumia selikinga kuzalisha virusi wengine.
Wanasayansi hao walitoa kauli hizo za matumaini kukabili VVU mbele ya viongozi mashuhuri wa kisiasa, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton na Rais wa Ufaransa, Fran├žois Hollande.
Mtaalamu anayesimamia mipango ya afya Ikulu ya Marekani, Profesa Antony Fauci, ambaye piya ni Mkurugezi wa taasisi ya nchi hiyo ya Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID), alikuwa miongoni mwa waliohutubia na kusifu hatua iliyofikiwa na wanasayansi duniani.
Ofisa Mkuu na Rais wa Taasisi ya Mapambano ya Ukimwi nchini Marekani, Phill Wilson aliweka bayana kuwa pamoja na ugonjwa huo kuonekana tishio hasa kwa nchi zinazoendelea, hakuna nchi, hata zile tajiri, ambazo zinaweza kutamba haziathiriki na tatizo hilo.
Kwa hivyo akasema mikakati na sera mpya za kisayansi zinahitajika dunia nzima, hivyo akawataka wanasayansi hao ‘kuanika hadharani silaha zao’ ili zianze kutumika ulimwenguni kote.
Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa wa Mapambano ya Ukimwi (UNAIDS), Sheila Tlou aliwataka wataalamu hao kuweka mkakati mzuri utakaowezesha silaha hizo za kisayansi kuelekezwa katika nchi maskini hasa barani Afrika.
Wanasayansi hao wamekuja na kauli hizo za matumaini wakati ambapo tayari wamefanya tafiti mbalimbali na kugundua tabia za VVU ikiwa ni pamoja na vitu ambavyo vinaviwezesha kushambulia seli nyeupe za damu, maarufu kwa jina la CD4, ambazo ni sehemu ya kinga ya mwili wa binadamu.
Licha ya tafiti mbalimbali kuonyesha kuwa kuna kila dalili ya kupatikana kwa chanjo, miaka michache iliyopita, waligundua moja ya dawa zinazotumika kupunguza makali ya VVU (ARV) ijulikanayo kama Truvada, yenye uwezo wa kumkinga mwathirika kumwambukiza mpenzi wanayeshiriki naye tendo la ndoa.
Wiki chache zilizopita, Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) iliidhinisha Truvada, ambayo ilianza kutumika sehemu mbalimbali duniani tangu mwaka 2004, kuwa ni tiba ya kuzuia kuenea kwa Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Kwa mujibu wa maelezo ya FDA, mwathirika anayetumia dawa hiyo anaweza kujamiiana na mwenza wake ambaye hana VVU bila kutumia kondomu na hatomwambukiza.
Matokeo ya utafiti huo wa ARV yaliwahi kuchapishwa kwenye gazeti hili toleo la Februari 12, mwaka huu. Kwa mujibu wa FDA, Truvada inatarajia kuanza kutumika na kusambazwa duniani katika kipindi cha miezi mitatu ijayo
source:mwananchi

Post a Comment

0 Comments