Wachezaji 17 wa timu
ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys)
wamefanyiwa vipimo vya kubaini umri wao halisi (MRI Tests) kwenye
hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Upimaji huo
ulifanyika Julai 14 mwaka huu chini ya usimamizi wa mjumbe wa Kamati ya
Tiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Dk. James Sekajugo
kutoka Uganda na Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Dk. Sylvester Faya.
Dk. Sekajugo alisema
vipimo hivyo vya Magnetic Resonance Imaging (MRI) vinafanya kutokana na
maelekezo ya CAF kwa nchi zote ambazo zitashiriki mashindano ya U17
ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Morocco ili kubaini umri
halisi wa wachezaji hao.
Amesema vipimo vya
MRI havina madhara kama ilivyo kwa X-ray ambapo vyenyewe vinachunguza
uimara wa mifupa ili kubaini umri halisi wa mchezaji, na uwezo wake ni
kubaini watu walio chini ya umri wa miaka 17.
CAF imeamua vipimo
hivyo vifanyike kabla ya wachezaji kuingia kwenye mashindano kwani
Afrika inakabiliwa na tatizo sugu la kudanganya umri wa wachezaji.
“Naipongeza TFF kwa
kuhakikisha upimaji unafanyika kama ilivyoagizwa na CAF. Wakati mwingine
si udanganyifu, unajua katika Afrika hakuna utaratibu wa watoto
kuandikishwa wanapozaliwa. Hivyo inawezekana kabisa mtoto au mzazi wake
hakumbuki au hajui tarahe aliyozaliwa,” amesema Dk. Sekajugo.
Amesema uamuzi wa
CAF kufanya vipimo vya MRI kabla ya wachezaji kuanza mashindano umelenga
kuhakikisha wachezaji wanaoshinda wana umri sahihi, badala ya vipimo
hivyo kufanyika wakati wa fainali.
“Mwaka 2005 CAF
iliamua kufanya vipimo hivyo miezi miwili kabla ya kuanza michuano ya
fainali. Kuna timu moja ilikutwa wachezaji wake wote wamezidi umri,
hivyo ikabidi waunde timu mpya,” amesema Dk. Sekajugo na kuongeza kuwa
matokeo ya vipimo vya wachezaji wa Serengeti Boys vitatumwa baada ya
wiki mbili.
Naye Dk. Faya ambaye
pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF amesema wachezaji 10
waliobaki watafanyiwa vipimo hivyo baadaye kabla ya mechi ya michuano
hiyo CAF dhidi ya Kenya itakayochezwa Septemba mwaka huu.
Wachezaji tisa wako
nchini Burundi kwenye michuano ya Rolling Stone Multipurpose Acre
Foundation wakati mmoja (Dickson Ambundo) amekwenda Ujerumani na timu ya
TASC ya Mwanza.
Walioko Burundi ni
Hamad Juma, Mgaya Jaffar, Ismail Gambo, Mohamed Hussein, Hussein
Ibrahim, Mudathir Abbas, Farid Shah, Joseph Lubasha na Kelvin Friday.
Dk. Faya amesema
vipimo vya MRI kupanywa mapema ni vizuri kwa sababu tatizo la
udanganyifu wa umri lipo, lakini pia litaisaidia TFF kwani inatumia
gharama kubwa kuandaa timu, hivyo ni vizuri ikaandaa timu ya wachezaji
wenye umri sahihi badala ya waliodanganya umri ambao hawataruhusiwa
kushiriki mashindano.
Mwaka 2005 Serengeti
Boys ilifuzu kucheza fainali za Afrika zilizofanyika Banjul, Gambia
lakini ilinyang’anywa nafasi hiyo baada ya kubainika kuwa baadhi ya
wachezaji wake walikuwa wamezidi umri wa miaka 17.
Boniface Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 Comments