Business

header ads

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MWANZA YAING’OA KINONDONI COPA COCA-COLA 2012
Mwanza imekata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola baada ya leo (Julai 11 mwaka huu) kuitoa Kinondoni kwa penalti 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
 
Hadi dakika 90 za mechi hiyo ya robo fainali zinamalizika timu hizo zilikuwa hazijafunga, hivyo kulazimika kuingia kwenye mikwaju ya penalti ili kupata mshindi ambaye atacheza nusu fainali keshokutwa (Julai 13 mwaka huu) dhidi ya Temeke.
 
Walioifungia Mwanza katika penalti ni Christopher Maghinwa, Steven Lubela na Juma Masunga. Penalti ya Kinondoni ilitiwa wavuni na Shabani Nyenje. Waliokosa kwa Kinondoni ni Miza Abdallah, John Komba na Juma Masunga.
 
Nusu fainali ya pili itakuwa kati ya Morogoro na mshindi wa mechi ya robo fainali kati ya Dodoma na Tanga itakayochezwa leo jioni (Julai 11 mwaka huu) kwenye uwanja huo huo.
 
WAAMUZI KAGAME KUNOLEWA JULAI 12
Mtihani wa utimamu wa mwili (fitness test) kwa waamuzi walioteuliwa kuchezesha michuano ya Kombe la Kagame inayoanza Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) utafanyika kesho (Julai 12 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Waamuzi 15 walioteuliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kuchezesha michuano hiyo. Waamuzi hao wanawasili leo jijini Dar es Salaam.
 
Kwa upande wa waamuzi wa kati (centre referees) ni Anthony Ogwayo (Kenya), Dennis Batte (Uganda), Israel Mujuni (Tanzania Bara), Issa Kagabo (Rwanda), Thierry Nkurunziza (Burundi), Farah Aden Ali (Djibouti) na Waziri Sheha (Zanzibar).
 
Waamuzi wasaidizi (assistant referees) ni Elias Kuloba (Kenya), Peter Sabatia (Kenya), Musa Balikoowa (Uganda), Hamis Changwalu (Tanzania Bara), Jesse Erasmo (Tanzania Bara), Simba Honore (Rwanda), Abdulahi Mahamoud (Djibouti) na Josephat Bulali (Zanzibar).
 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Post a Comment

0 Comments