TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Julai 20, 2012
UAMUZI KUHUSU SUALA
LA MCHEZAJI KEVIN YONDANI
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za wachezaji
(ambayo katika uamuzi huu itarejewa kama ‘Kamati’) iliyokutana Julai 17
mwaka huu, baada ya kupitia mikataba na nyaraka zote zinazohusiana na
mchezaji Kevin Yondani katika kujiridhisha juu ya hadhi yake ya usajili
katika mashindano ya Kombe la Kagame kama zilivyowasilishwa mbele yake
imefikia uamuzi ufuatao;
1. Kwa mujibu wa mapitio ya
nyaraka zote zilizotajwa hapo juu na kufanyiwa upembuzi yakinifu, Kamati
iliridhika pasi na shaka yoyote kuwa suala zima la mchezaji Kevin
Yondani ni la kiutendaji, hivyo uamuzi wa Sekretarieti ya TFF
kuwasiliana na Klabu ya Simba kwa suala hilo la kiutendaji
kama Sekretarieti ilivyofanya katika
barua yake ya Julai 14
mwaka huu ulikuwa sahihi.
2. Kamati
ilibaini kuwa Mkataba wa mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya Simba
ulimalizika Mei 31 mwaka huu. Hivyo kwa taratibu za usajili mchezaji
Kevin Yondani kuanzia Juni 1 mwaka huu alikuwa ni mchezaji huru.
3. Aidha
Kamati ilibaini kuwa Mkataba uliowasilishwa na Klabu ya Simba TFF ukiwa
na maana ya kuongeza mkataba uliokuwepo TFF baina ya mchezaji Kevin
Yondani na Klabu ya Simba uliwasilishwa TFF, Juni 7 mwaka huu ambapo ni
kinyume cha utaratibu wa kuongeza mikataba ya wachezaji unaozitaka klabu
kuwasilisha mikataba ya kuongeza muda wa mikataba ya wachezaji wao
wakati mkataba halisi haujaisha muda wake. Hivyo mkataba huo kwa jicho
la
kisheria haupo.
4. Hata
kama kamati ingeuona mkataba huo katika jicho la sheria, bado mkataba
huo una tatizo la kisheria hasa katika tarehe ambazo pande mbili husika
ziliingia makubaliano hayo. Ukiuangalia mkataba huo unabainisha kuwa,
wakati mchezaji Kevin Yondani aliingia makubaliano Desemba 23 mwaka
jana, upande wa pili wa kimkataba ambao ni Klabu ya Simba inaonekana
iliingia makubaliano hayo kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Geofrey
Nyange Kaburu,
Desemba 23 mwaka huu.
5. Kisheria
utata huu unaweza kuondolewa na pande husika tu kwa kurekebisha dosari
hiyo kwa maridhiano kuweka saini katika mabadiliko hayo ili kuthibitisha
mabadiliko hayo. Hivyo katika jicho la kisheria mkataba huo hauwezi
kutumika kumzuia mchezaji huyo kwenda katika klabu anayoipenda wakati
akiwa huru.
Kutokana na maelezo yote
hapo juu, Kamati imeridhia hatua iliyochukuliwa na Sekretarieti ya TFF
ya kumruhusu mchezaji Kevin Yondani kuichezea timu ya Yanga katika
mashindano ya Kombe la Kagame 2012.
Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 Comments