Business

header ads

SIMBA YAPOKEA UZI MPYA


                           TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


KLABU ya soka ya Simba jana imepokea msaada wa jezi, raba, viatu vya kuchezea mpira, mabegi na suti za michezo (tracksuit) – vyote vya kisasa kabisa, kutoka kwa familia ya Al Ruwahi. Msaada huo umetolewa kwa mapenzi mema ambayo familia hiyo inayo kwa klabu.

Ikumbukwe kwamba mahusiano baina ya familia ya Al Ruwahi (Ruwehi) na Simba yamedumu kwa zaidi ya miaka 30 sasa. Takribani miaka 30 iliyopita, familia hiihii ilitoa zawadi ya basi (Nissan Coaster) kwa Simba na kuifanya klabu yetu kuwa ya kwanza nchini kumiliki basi lake yenyewe.

Msaada huo wa sasa kwa Simba una thamani ya Sh milioni 18 kwa ujumla wake na Simba sasa itavaa jezi hizo katika pambano lake la kesho dhidi ya Azam katika michuano ya Kombe la Kagame.

Klabu ya soka ya Simba inatumia nafasi hii kuwakaribisha wapenzi na wanachama wake kujitokeza kuisaidia klabu kwa namna yoyote ile, kama ilivyofanya familia hii ya Al Ruwahi, ili kusukuma mbele gurudumu la  maendeleo ya klabu.

Simba ni ya kila mmoja na haina mwenyewe. Umoja na mshikamano baina ya viongozi, wadhamini, wapenzi na wanachama wake, ndiyo utakaoifanya izidi kuwa bora hapa nchini na nje ya mipaka ya taifa letu.

Kombe la Kagame

HALI za wachezaji waliopo katika kambi Hoteli ya Vina iliyopo Mabibo jijini Dar es Salaam inaendelea vizuri. Majeruhi ni mmoja tu, Amir Maftah na Abdallah Juma amefanyiwa vipimo jana na majibu yake yanatolewa baadaye leo.

Kwa mujibu wa CECAFA, wachezaji wote waliokuwa na kadi moja ya njano kwenye hatua ya makundi wamefutiwa kadi zao na hivyo Simba itaingia uwanjani kesho Jumanne kwenye pambano dhidi ya Azam ikiwa haina mchezaji mwenye adhabu.

Simba imesifiwa na CECAFA kuwa ni miongoni mwa timu zenye nidhamu nzuri kwenye michuano ya Kagame mwaka huu, mfano ukitolewa kwenye pambano lake dhidi ya AS VITA ya DR Congo, ambapo hakukuwapo na kadi yoyote iliyotolewa mechi nzima.

Wenu

Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC

Post a Comment

0 Comments