Business

header ads

LULU APANDISHWA KIZIMBANI KISUTU


Elizabeth Michael Kimemeta


MSANII wa filamu nchini, Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu (17), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na shtaka la mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Lulu ambaye alikuwa amevalia dira la rangi ya njano, kandambili za rangi nyekundu na kujifunika mtandio wa rangi ya pinki, alifikishwa mahakamani hapo jana saa 4:00 asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi wawili wa kike na mmoja wa kiume.

Lulu alipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Elizabeth Kaganda, akimsomea hati ya mashtaka alidai kuwa Aprili 7 mwaka huu, maeneo ya Sinza Vatcan, Lulu alimuua, Steven Kanumba.

Alisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama iipangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. Kesi hiyo itatajwa tena Aprili 23.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Lulu hakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo ya mauaji. Kesi za mauaji zinasikilizwa na Mahakama Kuu.

Hakimu Mmbando aliamuru Lulu apelekwe rumande katika Gereza la Segerea kwa sababu shtaka linalomkabili ni moja kati ya mashtaka yasiyo na dhamana.

Mahakamani jana

Msanii huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa gari ndogo na kuwapa wakati mgumu waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo.

Waandishi walikuwa wametanda karibu kila kona ya mahakama hiyo na Mahakama ya Watoto ili kuweza kumuona akipandishwa kizimbani.

Askari wa kike aliyevalia nguo za kiraia alimtoa Lulu ndani ya gari hilo, huku akiwa amejifunika mtandio usoni kwa kumshika mkono kama mtu na rafiki yake na kumwingiza mahakamani kupitia mlango wa nyuma.

Hata baada ya waandishi wa habari kubaini janja hiyo, waliendelea kupata vikwazo kutoka kwa askari polisi aliyekuwepo mlangoni ambaye aliwazuia wasiingie.

Baada ya muda mrefu wa majadiliano, waandishi waliingia ndani ya chumba cha mahakama lakini mtihani mwingine ukawa kwa wapigapicha kwani wengi walizuiwa kutimiza jukumu lao hilo.

Lulu alisomewa mashtaka yake haraka na kutolewa tena akiwa chini ya ulinzi mkali huku akifichwa asipigwe picha.

Kanumba alifariki dunia April 7 saa 9:00 usiku kwa kile kilichodaiwa kuwa ni baada ya ugomvi baina yake na Lulu. Alizikwa juzi kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments