Business

header ads

KANUMBA ALIJITABIRIA KIFO FILAMU YAKE YA MWISHO
Marehemu Steven C Kanumba

MPIGA picha na mhariri wa filamu za Steven Kanumba, Zakayo Magulu amesema kifo cha msanii huyo kinafafana na hadithi ya filamu yake ya mwisho aliyoigiza, inayoitwa Price of Love ambayo bado haijatolewa.Mugulu alisema hayo jana alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza Vatican, Dar es Salaam.Alisema filamu hiyo ambayo Kanumba aliibadilisha jina na kuiita Power and Love inaeleza jinsi msanii huyo alivyotoa figo na baadaye kufa baada ya kusukumwa na mpenzi wake katika filamu hiyo ambaye alikuwa ni Irene Paul.

Akiielezea filamu hiyo ambayo bado haijatoka licha ya kuwa imeshakamilika, alisema Kanumba aliigiza kama mtu maskini aliyempenda msichana ambaye alikuwa na uhusiano na mwanamume tajiri.

“Katika filamu ile Kanumba alitoa figo yake moja baada ya huyo msichana (mpenzi wake) kuugua na kutakiwa kuwekewa figo nyingine. Alipotoa Figo uliibuka ugomvi baina yake na mpenzi wake ambaye alimsukuma na Kanumba alianguka na kuumia. Baada ya tukio hilo, alikimbizwa hospitali na baada ya muda mfupi alifariki dunia.”

Alisema msanii, Idrisa Makupa maarufu kama Kupa ndiye aliyeona kifo cha Kanumba katika filamu hiyo na pia hata baada ya kifo chake, ndiye mtu wa mwisho kuuona mwili wa Kanumba ukiingizwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuufunika…. “Ni mambo ya ajabu.”
Alisema hata daktari aliyemfanyia operesheni Kanumba katika filamu hiyo ndiye huyo huyo aliyefika nyumbani kwa Kanumba kumpatia huduma baada ya kuanguka.

Alisema tukio la kifo cha Kanumba katika filamu hiyo iliyoandikwa na Ali Yakuti halikuwepo ila liliongezwa na msanii huyo mwenyewe… “Filamu hiyo ilikuwa na matukio (scene) 84 lakini, yalibadilishwa matukio 40 likiwemo la kifo chake.”

Mchaguaji wa maeneo ya kupigia picha za filamu za Kanumba, Rahim Khatib maarufu kama Kiuno alisema katika filamu hiyo ya mwisho ya msanii huyo alipendekeza picha zipigwe katika maeneo yenye giza na mwanga halisi (usio wa taa).

Mtoto wa Kanumba
Katika hatua nyingine imebainika kuwa Kanumba (28), ameacha mtoto mmoja wa kiume.Akizungumza jana nyumbani kwa marehemu, mama mzazi wa msanii huyo, Flora Mtegoa alisema: “Kama kuna aliyezaa na mwanangu ajitokeze na familia itamsikiliza.”

Taarifa za Kanumba kuacha mtoto zilikuwa gumzo jana nyumbani kwa marehemu ambako baadhi ya ndugu walioonekana kufurahia na wengine kupinga wakidai kuwa mtoto huyo na marehemu.

Hata hivyo, baada ya mama huyo kutoa kauli hiyo dada yake marehemu Kanumba, Abella Kajumulo alisema mtoto huyo si wa mdogo wake kwa sababu katika uhai wake Kanumba hakuwahi kuieleza familia yake kama ana mtoto wala mke.

“Mbona huyo mwanamke hakujitokeza wakati wa msiba wa Kanumba aje kujitokeza hivi sasa? Niliwahi kumwuliza (Kanumba) juu ya ndoa yake na kama ana mtoto alikataa kabisa akasema hana mtoto wala mke,” alisema Kajumulo.Wakati ndugu hao wakibishana kuhusu habari hizo, aliibuka kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Patrick Kamwele na kuwaeleza kuwa mtoto huyo ni wa Kanumba na kwamba anamfahamu vizuri msichana huyo.

Kamwele ambaye ni raia wa Kenya aliingia mkataba na kampuni ya Kanumba The Great tangu mwaka 2009 na katika mazungumzo yake na ndugu hao aliwaeleza kuwa atakuwa shahidi iwapo atahitajika kufanya hivyo.

Alisema mara ya kwanza kumwona msichana huyo ilikuwa Septemba 2009, baada ya kufika nyumba kwa Kanumba kwa ajili ya kufanya mazungumzo kabla ya kuingia naye mkataba.

“Baada ya kukaa nyumbani kwa Kanumba kwa muda wa wiki mbili huyo msichana, alianza kuumwa na Kanumba alimpeleka hospitali na alibainika kuwa ni mjamzito,” alisema Kamwele.

Alifafanua kwamba baada ya msichana huyo kusema kuwa mimba hiyo ni ya Kanumba, yeye pamoja na baadhi ya wasanii wa bendi ya muziki wa dansi ya FM Academia, waliitwa katika kikao na msanii huyo.

“Katika kikao kile tulimhoji msichana huyo na alisema mimba ni ya Kanumba, ila baadaye msichana huyo aliondoka ingawa mimi sijui kama alifukuzwa au aliondoka mwenyewe,” alisema.

Alisema kilichoendelea baada ya hapo hakukijua mpaka alipokuja kuiona habari hiyo katika gazeti jana.

Mmoja wa wasanii wa filamu ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema anamfahamu msichana huyo na kwamba alikuwa mfanyakazi wa ndani wa Kanumba.

Msanii huyo alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na Kamwele mbele ya ndugu zake Kanumba, huku akitizama picha ya msichana huyo katika gazeti na alisema: “Namfahamu huyu msichana alikuwa msichana wa kazi wa Kanumba.”

Kamwele aliwataka ndugu wa marehemu Kanumba kulichukulia suala hilo kwa umakini kwa kuwa hawawafahamu watu wote waliokuwa wa karibu wa msanii huyo.“Mimi nimekaa na marehemu Kanumba kwa muda mrefu na ninawajua waliokuwa watu wake wa karibu akiwemo huyo msichana, nawashauri kulipa uzito suala hili,” alisisitiza Kamwele.

Familia yatoa utaratibu
Katika hatua nyingine, mama wa marehemu Kanumba amewaomba radhi wananchi wote kwa kitendo cha kukatisha ratiba za kuuaga mwili wa msanii huyo juzi katika Viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.

Mutegoa alisema ratiba hiyo ilikatishwa kutokana na watu kuwa wengi na kusababisha kuibuka kwa vurugu… “Sikutegemea kama watu wangekuwa wengi kiasi kile mpaka wengine kufikia hatua ya kupoteza fahamu… nawaomba radhi wote waliofika, pamoja na hayo wingi ule wa watu ulinipa faraja kubwa. Wameonyesha upendo wa hali ya juu.”

Kanumba alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi ya Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake Sinza Vatican huku taarifa za awali zikieleza kuwa kifo chake kilitokana na ugomvi na aliyekuwa mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’.
SOURCE: MWANANCHI

Post a Comment

0 Comments