Business

header ads

UONGOZI MKOANI RUVUMA UMESIKITISHWA NA MAANDAMANO YA VIJANA YASIYO HALALI
ASKARI FFU WAKIMSHIKILIA MMOJA WA VIJANA WALIOKUWA WAKRUSHA MAWE KATIKA MPAMBANO HUO WA POLISI NA WAKAZI WA SONGEA.
POLISI WAKIONDOA MAGOGO YALIYOWEKWA BARABANI NA VIJANA KUPINGA WENZAO WALIOUAWA NA WATU WASIOJULIKANA KATIKA MAENEO MBALIMBALI MJINI SONGEA.
Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia FFU wakiwa wamewaweka chini wananchi waliokuwa kaika maandamano hayo

Akitoa tamko hilo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ameeleza kuwa kwa muda wa siku tatu zilizopita kumekuwepo na tetesi za kutokea mauaji kwa imani za kishirikina zenye kulenga zaidi akinamama kuondoa sehemu za mwili kuwasaidia mambo ya kibiashara hivyo kupelekea watu kufariki.


Kufuatia matukio hayo mkoa uliagiza Jeshi la polisi kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo kwa kufanya uchunguzi wa wanaojihusisha na mauaji hayo kazi inayoendelea hadi sasa. Katika maandamano ya leo watu wawili wamefariki dunia kwa kupigwa risasi wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji hao waliokuwa wakiwarushia mawe polisi wa kutuliza ghasia.


Aidha Mkuu wa mkoa amewasihi wananchi wa Songea na Ruvuma kwa pamoja wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu ili vyombo vya ulinzi na Usalama viendelee kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha wote wanaojihusisha na biashara hii haramu wanachukuliwa hatua za kisheria.Ametoa wito wananchi kuwabaini watu wanaondesha uhalifu kwa njia ya uchawi na ushirikina na ambao wanaishi katika Mitaa yetu kwa kutoa taarifa zao kwa viongozi wa Mitaa na vyombo vya ulinzi na Usalama mapema.


“Serikali haimini kuhusu ushirikina wala uchawi.Inaelewa kuhusu tiba asilia na kwa tiba hizi hufanywa na watu wanaopewa vibali na serikali” alisema na kusisitiza kuwa wananchi wa Ruvuma wakatae ushirikina wa kiwango hicho pia uendeshaji wa ramli chonganishi zenye lengo la kugombanisha ndugu,jamii na Taifa kwani madhara yake ni kutokea mauaji kama haya kwa wasio na hatia.


Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa wananchi wa Ruvuma kutoa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na Usalama katika kipindi hiki kwa kuwabaini wote wanaojihusisha na kuendeleza uhalifu huu kwa vigezo vya uchawi na ushirikiana.


Amewaagiza watendaji wa Mitaa,kata na Tarafa kuhakikisha ulinzi kwa kushirikiana na Polisi wanaendesha operesheni katika Mitaa yote na nyumba za kulala wageni ili kuwabaini wahalifu wote huku hatua za kisheria zikichua mkondo.


“Sote tukiungana hawa wachawi,waganga wa jadi na majambazi wanaodandia humo tunaweza kuwadhibiti ili mauaji yakome na Songea irudie utulivu wake kama kawaida” alisema Mkuu wa Mkoa.


Kwa mujibu wa taarifa za polisi jumla ya watu watano hadi sasa wameripotiwa kuuwawa kwa hisia za ushirikina na uchawi katika maeneo ya Lizaboni, Bombambili na Matarawe kati yao wanawake watatu na wanaume wawili.Hata hivyo kati yao hakuna hata mmoja aliyeondolewa kiungo cha mwili kama wanavyodia baadhi ya wananchi waliondamana.


Post a Comment

0 Comments