Business

header ads

Mauaji ya kinyama Mbozi

NI tukio la kusikitisha na kuleta simanzi ambalo limetokea katika familia ya Mzee Jackson Mwashiuya(78) na wakazi wa mtaa wa Ichenjezya mjini Vwawa wilayani Mbozi mkoani Mbeya baada ya mjukuu wake Dominick Mwashiuya kutekwa na watu wasiofahamika kisha kumuua kikatili kwa kukatwakatwa viungo vyake vya mwili na kutelekezwa katika chumba cha kuuzia pombe za kienyeji.

Tukio hiolo la Mauaji ya kusikitisha limetokea Ijumaa majira ya saa 11 jioni ambapo marehemu aliitwa na mmoja wa wanawake wanaouza pombe ya Ulanzi katika kilabu maarufu ya pombe za kienyeji inayofahamika kwa jina la ’Kwa Jimmy’ambapo muda mfupi baadaye marehemu alikutwa akiwa amekufa huku mwili wake ukiwa umetapakaa damu.

Mwili huo wa marehemu ulikutwa katika chumba kilichoandikwa ‘Ikumbilo Kilabu’ ambapo muuzaji wa chumba hicho mwanamke aliyefahamika kwa jina moja la Nampashi alitoweka na watu wasiofahamika wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo.

Babu wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Mzee Jackson Mwashiuya alisema kuwa, majira ya saa 11 jioni alikutana na mwanaye aliyefahamika kwa jina la Maria ambapo muda mfupi baadaye marehemu ambaye ni mjukuu wake wa mtoto wa kiume alikuja kwa ajili ya kumsalimia shangazi yake.

Mzee Mwashiuya alisema kuwa wakati mjukuu wake akisalimiana na shangazi yake mara alifika mwanamke anayeuza ulanzi katika chumba kilichoandikwa ‘Ikumbilo Kilabu’ anayefahamika kwa jina moja la Nampashi ambaye alimuita marehemu na kwenda naye katika chumba anachouzia pombe aina ya ulanzi.

Alisema kuwa yeye aliondoka na kuingia katika chumba kingine kilichopo Kilabuni hapo ambapo alijumuika na watu wengine katika burudani ya kunywa pombe za kienyeji bila kujua kinachoendelea katika chumba cha pili ambacho kimepakana na chumba walichokuwa wameketi wao.

‘’Sikujua kinachoendelea katika chumba cha pili nilikaa na wazee wenzangu tunakunywa komoni, baadaye walifika watu kutueleza kuwa kuna mtu ameumizwa chumba cha pili…wote tulitoka ndani na kusimama nje ya chumba alichofia marehemu bila kujua ni nani aliyemo humo ndani,’’alisema Mzee Mwashiuya.

Alisema kuwa walichungulia katika chumba hicho na kuona miguu na damu ikiwa inachuruzika na kwamba kwa kuwa chumba kilikuwa na giza hawakuweza kuutambua vyema mwili wa marehemu kwa wakati huo.

Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa mtaa wa Ipanga ambao umepakana na mtaa wa Mpakani lilipotokea tukio Bw.Joseph Lwenje alisema kuwa mara baada ya kupata taarifa za tukio hilo aliingia katika chumba hicho na kumulika kwa kurunzi ambapo alikutana na dimbwi la damu huku mwili wa marehemu ukiwa na majeraha makubwa.

Alisema kuwa alitoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa mtaa wa Bw.Tuliani Mwahalende ambaye aliondoka pamoja na mmoja wa wazee wa kamati ya ulinzi na usalama ya mtaa huo Bw.Herman Mpinga hadi kituo cha Polisi na kutoa taarifa za tukio hilo na askari polisi walifika eneo hilo na kuukagua mwili wa marehemu ndipo ilipofahamika kuwa aliyeuawa ni mjukuu wa Mzee Mwashiuya.

Kwa upande wake baba wa marehemu Bw.Richard Mwashiuya alisema kuwa alifika eneo la tukio muda mfupi mara baada ya kusikia minong’ono ya kuwepo mtu ndani ya chumba alichofia lakini hakujua kama aliyeuawa kuwa ni mwanaye ambaye ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wake sita.

Alisema kuwa mara baada ya kutokea mauaji hayo kumeibuka tetesi kuwa kijana wake alikuwa akishiriki mapenzi na mwanamke anayeuza pombe za kienyeji ambapo pia inadaiwa kuwa mwanamke huyo alikuwa na mwanaume mwingine ambaye pia alikuwa akihusiana naye kimapenzi.

Baba mzazi wa marehemu alisema kuwa walishiriki katika kuukagua mwili wa marehemu katika hospitali ya wilaya ya Vwawa ulikohifadhiwa na kubaini majeraha makubwa ya kukatwa na kitu chenye ncha kali ambapo viganja vya mikono yake na vidole viliachana huku sehemu ya fuvu lake la kichwa ikiwa imefumuka kiasi cha kuonekana ubongo.

Alisema mazishi ya kijana wake yalifanyika katika makaburi ya Isangu yaliyopo Vwawa wilayani Mbozi majira ya saa tisa alasiri.

Aidha kufuatia mauaji hayo kamati ya ulinzi ya mitaa miwili ya Mpakani na Ipanga ilikusanyika kujadili tukio hilo na kufikia uamuzi wa kufunga Kilabu hicho cha pombe za kienyeji kutokana na kuonekana kuwa eneo hilo limekuwa ni chanzo cha uhalifu.

Akizungumzia kufungwa kwa Kilabu hicho Kaimu Mwenyekiti wa Mtaa wa Mpakani Bw.Danford Mhema alisema kuwa kamati ya ulinzi na usalama ya mtaa iliketi na kujadili na hatimaye kugundua kuwa Kilabu hicho mbali na kuuza pombe za kienyeji ni danguro la ngono na uvutaji wa dawa za kulevya ambalo pia linaficha wahalifu.

Alisema kuwa eneo hilo pia ni maarufu kwa uchezaji wa kamari ambapo pia Kilabu hicho kinakesha hadi usiku wa manane jambo ambalo limekuwa kero kwa wakazi wa maeneo hayo huku mmiliki wa eneo hilo Bw.Jimmy Mwamlima akishindwa kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyofanyika katika Kilabu chake.

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na linafanya uchunguzi kuwanasa wauaji ili kuwafikisha mikononi mwa sheria.

Post a Comment

0 Comments